Wanaotaka kujitenga Yemeni wadhibiti mji wa Aden
11 Agosti 2019Wanaotaka kujitenga wakiungwa mkono na Umoja wa falme za Kiarabu UAE wamekuwa wakipigana kama sehemu ya muungano unaoongozwa na saudi Arabia ambao unaounga mkono serikali lakini wameyageuka majeshi hayo katika mapigano katika mji huo wa kusini. Idadi ya watu waliofariki katika mapigano ya siku nne imepanda na kufikia zaidi ya watu 70, ikiwa ni pamoja na raia, maafisa hao wamesema.
Matukio ya hivi karibuni yanaweza kuvuruga zaidi muungano huo ambao umekuwa ukipambana na waasi wa Kihouthi ambao ni washirika wa Iran tangu mwaka 2015 kwa niaba ya serikali ya rais Abed Rabbo Mansour Hadi , ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa katika mji wa Aden tu. Wahouthi wanadhibiti upande wa kaskazini pamoja na mji mkuu Sanaa.
Kanali Turki al-maliki , msemaji wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, alinukuliwa jana katika shirika la habari la serikali ya Saudia akisema kuwa "uongozi wa pamoja wa muungano unatoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika mji mkuu wa mpito wa Yemen, Aden, na utatumia nguvu za kijeshi dhidi ya wale watakaokiuka hatua hiyo."
Amesema muungano huo wa kijeshi unatoa wito kwa baraza la mpito la wanaotaka kujitenga upande wa kusini pamoja na majeshi ya ukanda wa usalama "kurejea mara moja katika maeneo yao na kujiondoa kutoka katika maeneo yote waliyoyakamata katika muda wa siku chache zilizopita."
Mkutano wa dharura
Maafisa wa usalama mjini Aden , ambao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwasababu hawana mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari, wamesema majeshi ya Saudia yamekuwa yakilinda ofisi ya Hadi na mawaziri wake katika jengo la makao ya rais, lakini majeshi ya ulinzi wa kanda ya usalama yako nje ya jengo hilo.
Wamesema kiasi ya walinzi 300 wa jengo la rais waliruhusiwa kuondoka katika eneo hilo , na waziri wa mambo ya ndani Ahmed al-Maisari pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi waliondolewa na kupelekwa nchini Saudi Arabia siku ya Jumamosi.
Wanaotaka kujitenga pia wamekamata kambi ya jeshi katika eneo la kati la Khormaksar, wamesema.
Saudi Arabia imezialika pande zinazopigana mjini Aden kwa ajili ya "mkutano wa dharura" nchini Saudi Arabia , kwa mujibu wa shirika la habari la Saudi Arabia.
Wanaotaka kujitenga baadaye walisema katika taarifa fupi wamekubali kusitisha mapigano na mwaliko wa mkutano.
Mapigano yalizuka siku ya Jumatano wakati majeshi tiifu kwa baraza la mpito la eneo la kusini yalipojaribu kuingia katika jengo la rais mjini Aden baada ya waziri wa zamani Hani Bin Braik , naibu mkuu wa kundi hilo la STC, kutoa wito kwa serikali ya Hadi kupinduliwa.