Wanamgambo wa kikurd walihama eneo linalopakana na Uturuki
23 Oktoba 2019Waziri wa ulinzi wa Marekani amepangiwa kukutana na waziri mwenzake sawa na waziri mkuu Adel Abdul Mahdi kuzungumzia mpango wa kuwaondowa wanajeshi wa Marekani nchini Syria na nafasi inayoweza kushikiliwa na Iraq katika mpango huo.
Viongozi wa kijeshi wa Iraq walisema hapo awali wanajeshi wa Marekani wanaovuka mpaka na kuingia Iraq kama sehemu ya hatua za kuihama Syria hawana ruhusa ya kubakia na kwamba wataweza kusalia huko kwa muda tu.
Ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani inafuatia pia makubaliano yaliyofikiwa Sochi kati ya rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na rais Vladimir Putin wa Urusi yanayozungumzia juu ya kuwekwa wanajeshi wa nchi hizo mbili kaskazini mashariki mwa Syria ili kuwaondowa wapiganaji wa kikurd na silaha zao kutoka mpaka wa Uturuki.
Wakaimbizi wa Syria kurejeshwa katika eneo salama kaskazini mashariki mwa Syria
Masaa machache baada ya makubaliano hayo kutangazwa, wizara ya ulinzi ya Uturuki ilisema Marekani imeiarifu Uturuki kuhusu kukamilika zoezi la kuhama wanamgambo wa kikurd katika lile eneo la Usalama Uturuki inalodai litengwe kaskazini mwa Syria.
Kukamilika zoezi la kuhama wanamgambo wa kikurd YPG, kama kutathibitishwa, itamaanisha ushindi kwa rais Erdogan aliyeanzisha Oktoba tisa iliyopita hujuma za kijeshi ili kuwatimua wanamgambo hao kutoka eneo la karibu na mpaka wake na kufungua eneo salama kwaajili ya wasyria watakaorejeshwa nyumbani."
Makubaliano kati ya Uturuki na Urusi yaliyofikiwa katika mji wa mwambao wa bahari nyeusi-Sochi yanaidhinisha pia mpango wa kurejea wanajeshi wa rais Bashar al Assad katika eneo la mpakani kwa ushirikiano pamoja na vikosi vya Urusi, wakikamata nafasi ya vile vikosi vya Marekani vilivyokuwa vikipiga doria kwa miaka kadhaa katika eneo hilo pamoja na washirika wao wa kikurd.
Urusi imeonya wanamgambo wa kikurd watakaosalia katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Syria ambalo litakuwa likisimamiwa na wanajeshi wa Urusi na Uturuki "watavunjwa nguvu".
Makubaliano kati ya Uturuki na Urusi yanatarajiwa kuanza kuifanya kazi jumatano mchana.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga