Wanajeshi watano wa Israel wauawa kusini mwa Lebanon
7 Novemba 2024Wanajeshi watano wa Israel wameuwawa na wengine 16 kujeruhiwa wakiwa mapambanoni kusini mwa Lebanon katika wiki za hivi karibuni. Haya ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Israel leo.
Taarifa hii inakuja wakati ambapo Israel imeendeleza mashambulizi yake ya makombora kwenye eneo la kusini la mji mkuu wa Lebanon Beirut, mapema leo, likiwemo eneo lililo karibu na uwanja wa ndege wa pekee wa kimataifa wa Lebanon.
Jeshi la Israel lilikuwa limetoa notisi ya watu kuondoka katika eneo hilo, likidai kulikuwa na vifaa vya wanamgambo wa Hezbollah katika eneo hilo. Israel na Hezbollah zashambuliana kwenye maeneo muhimu
Wakati huo huo Israel leo imepitisha sheria inayoweza kushuhudia jamaa za watu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya "kigaidi" kufukuzwa kutoka nchini humo na kupelekwa katika Ukanda wa Gaza ambako vita vinarindima.
Sheria hii imezua hofu miongoni mwa wanaharakati walio wachache wa Kiarabu. Wanasiasa wa mrengo wa kulia wamekuwa wakishinikiza kupitishwa kwa sheria hiyo kwa miaka, wakiamini itawazuia raia wa Palestina walio Israel na wakaazi wa Jerusalem mashariki kutofanya mashambulizi dhidi ya Waisraeli.