Wanajeshi wanaomska Kony wanahitaji vifaa
27 Juni 2012Umoja wa Mataifa unataka kikosi cha Umoja wa Afrika kinachomsaka kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, LRA, Joseph Kony, wapewe vifaa kamili kufikia mwezi Desemba mwaka huu. mjini New York.
Kikosi hicho cha Umoja wa Afrika kinachoungwa mkono na Marekani, kinalenga kuwa na wanajeshi 5,000 kutoka Sudan Kusini, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Uganda, lakini hakina vifaa, mafunzo, chakula na usafiri.
"Wanajeshi hawana karibu kila kitu. Hawana viatu, sare za kijeshi, chakula na wakati mwingine mafunzo," amesema Francisco Madeira, mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika anayehusika na masuala ya kundi la LRA, wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani jana. Madeira alisema kuna haja ya vitu hivi kutolewa.
Mjumbe huyo alisema nchi hizo nne zimeahidi kutoa wanajeshi hao na watapelekwa kumsaka Kony mara tu watakapokuwa na vifaa vya kutosha kuwawezesha kukaa huko. Alisema hawataki kuwatuma wanajeshi watakaokwenda kukaa bila kazi kwa kuwa wanaweza kugeuka kuwa wanyang'anyi. Alidokeza kwamba kuna umuhimu wa wanajeshi kuwa na maadili ya heshima na wafundishwe kuwahudumia raia na wala sio kuwa wanajeshi watakaojihudumia wenyewe na kunufaika kutoka kwa raia.
Madeira amesema kutahitajika juhudi thabiti za makusudi kulichakaza kabisa kundi la LRA na kuzisaidia jamii zilizoathiriwa. "Nadhani tunachokifanya sasa ni kuhakikisha tunarejesha kasi na kuuambia ulimwengu kuwa hali haijabadilika. Watu wanakufa. Watu wanahitaji msaada na muhimu zaidi ni usalama."
Madeira alisema kundi la LRA liko katika eneo kubwa kama nchi ya Ufaransa kwenye mpaka kati ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan Kusini na Jamuhuri ya Afrika ya Kati.
Mkakati kuwasilishwa kwa baraza la usalama
Abou Moussa, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa ofisi ya umoja huo kwa ajili ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati, anatarajiwa kulihutubia baraza la usalama la umoja wa Mataifa leo juu ya mkakati wa umoja huo wa kukabiliana na kitisho na athari za kundi la LRA.
Madeira na Moussa watakutana na wajumbe wa serikali za Ulaya, Marekani na Afrika leo kuomba msaada. Wajumbe hao walisema msaada mkubwa unahitajika katika kuwalinda raia katika maeneo yanayodhibitiwa na LRA, kuwashawishi waasi waliokimbia kundi hilo na kuzisaidia serikali kuanzisha mamlaka katika maeneo hayo.
Madeira anasema, "Tunahitaji kuwasaidia wale waliolikimbia kundi la LRA. Hiki ni mojawapo ya kipengee muhimu cha mkakati wetu, kuwajumisha katika jamii waliojitolea kuacha mapigano msituni."
Mkakati huo uliopatikana na shirika la habari la Reuters unazitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika kuhakikisha kikosi cha Umoja wa Afrika kina vifaa vya kutosha, pamoja na kuimarisha uwezo wake kufanya operesheni za angani, mawasiliano, kuwa na majengo ya ofisi na makazi, msaada wa matibabu, mafuta na chakula haraka iwezekanavyo na sio baada ya mwezi Desemba mwaka huu. Wanadiplomasia wanasema baraza la usalama linatarajiwa leo kutoa taarifa kuuridhia mkakati huo.
Usalama wa raia kulindwa
Mkakati huo uliopendekezwa unasema mafunzo kwa wanajeshi kuhusu kuheshimu haki za binaadamu, sheria za kimataifa za haki za binaadamu na kuwalinda raia, ni mambo yanayotakiwa kupewa kipaumbele.
"Kuna mahali popote duniani ambako tungeweza kulivumilia kwa robo karne kundi la aina hii linaloteka nyara, kukata viungo, kuua, kuwatisha raia na kuwalenga watoto miaka nenda miaka rudi?" Aliuliza kwenye mkutano wa jana wa New York, Jan Egeland, naibu mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, ambaye ni Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa aliyehusika na utoaji wa misaada ya kibinaadamu.
Kony, anayeshutumiwa kwa mauaji kaskazini mwa Uganda kwa miaka 20, anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague, Uholazni, kujibu mashitaka ya uhalifu wa kivita. Kundi lake la LRA linashutumiwa kwa kuwateka nyara watoto na kuwatumia kama wanajeshi na watumwa wa ngono na pia kuwakata viungo mateka wake kama mbinu ya kuwatisha na kulipa kisasi.
Mwandishi Josephat Charo/REUTERS/AFPE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir