Wanajeshi wa Korea Kaskazini wavuka mpaka wa ulinzi mkali
18 Juni 2024Wanajeshi kadhaa wa Korea Kaskazini wameripotiwa kuvuka mpaka wenye ulinzi mkali hii leo, na kurejea nchini mwao muda mfupi baada ya Korea Kusini kufyatua risasi za kutoa tahadhari.
Jeshi la Korea Kusini limesema linaamini kwamba kisa hicho cha Jumanne ni cha bahati mbaya, baada ya wanajeshi kati ya 20 hadi 30 wa Korea Kaskazini waliokuwa wamebeba vifaa vya kazi kuvuka mpaka, mwendo wa saa za asubuhi majira ya nchini humo.
Kulingana na Korea Kusini, hii ni mara ya pili kwa wanajeshi hao kuvuka mpaka katika kipindi cha wiki mbili, wakati Korea kaskazini ikiimarisha mipaka baina yake na Korea Kusini.
Katika tukio hilo, wanajeshi kadhaa wa Korea Kaskazini walijeruhiwa baada ya kulipukiwa na bomu la ardhini, Muungano wa Wakuu wa Jeshi mjini Seoul ulisema.