1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Wanajeshi wa Israel waua 104 kituo cha msaada Gaza

29 Februari 2024

Vikosi vya Israel vimeufyatulia risasi umati wa Wapalestina kwenye kituo cha kutoa msaada na kuuwa watu 104.

https://p.dw.com/p/4d2Tj
Mzozo wa Mashariki ya Kati | Hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa huko Deir El-Balah
Wapalestina waliojeruhiwa wakifikishwa hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa, Deir El-Balah.Picha: Ali Hamad/APA Images via ZUMA Pres/picture alliance

Vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya kwa vita  vimeufyatulia risasi umati wa Wapalestina kwenye kituo cha kutoa msaada hii leo, na kuwauwa watu 104 huku wengine zaidi ya 700 wakijeruhiwa. Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Kipalestina.

Duru za Israel zimethibitisha kuwa askari waliufyatulia risasi umati huo, wakiamini kuwa walikuwa tishio. Wizara ya afya ya Kipalestina huko Gaza imelaani kile ilichokiita kuwa ni mauaji ya kikatili.

Mzozo wa Mashariki ya Kati | Hospitali ya Mashahidi ya Al-Aqsa huko Deir El-Balah
Ndugu akilia baada ya kuiona maiti ya mpendwa wake.Picha: AFP/Getty Images

Shuhuda ameliambia shirika la habari la AFP vurugu zilianza wakati maelfu ya watu waliokuwa na hamu ya kupata chakula waliyakimbilia malori ya misaada katika eneo la magharibi mwa mji huo la Nabulsi.

Jeshi la Israel awali lilisema kuwa wakati wa kuingia kwa malori ya misaada kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, wakaazi wa Gaza waliyazingira na kupora bidhaa zilizokuwa zimewasilishwa.

Liliongeza kuwa wakati wa tukio hilo, wakaazi kadhaa wa Gaza walijeruhiwa kutokana na kusukumana na kukanyagana na tukio hilo liko chini ya uchunguzi.