Wanajeshi wa Ethiopia waamriwa kutokuingia Tigray
24 Desemba 2021Wanajeshi wote wa Ethiopia walio kwenye uwanja wa mapambano wameamriwa kusalia kwenye maeneo waliyokwishayakomboa kutoka kwa wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF), lakini sio kwenda mbele zaidi ndani ya jimbo la Tigray, alisema mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali ya Ethiopia, Legesse Tulu.
Jeshi la shirikisho la Ethiopia na washirika wake wamepata mafanikio makubwa ndani ya wiki za hivi karibuni, wakiichukuwa tena miji mikubwa na midogo katika mikoa jirani ya Amhara na Afar, ambayo wapiganaji wa Tigray walikuwa wameitwaa mapema mwaka huu. Vikosi vya TPLF vimelazimika kurudi nyuma kwenye jimbo lao.
"Awamu ya opereshani ya kuliondosha kundi la kigaidi kutoka kwenye maeneo lililoyavamia imekamilika kwa ushindi. Kwa sasa, hamu na uwezo wa adui kupambana umeharibiwa vibaya vibaya," alisema Legesse.
"Serikali itachukuwa hatua zaidi kuhakikisha kwamba hamu hiyo ya vikosi vya Tigray haiji tena juu siku zijazo. Kwa sasa, wanajeshi wa Ethiopia wanaamriwa kushikillia maeneo ambayo tayari wanayadhibiti," alisema msemaji huyo wa serikali.
Mwanzo wa mwisho wa vita?
Tangazo hilo la serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwamba wanajeshi wake hawatapambana tena na vikosi vya Tigray ndani ya jimbo lao inaweza kuwa hatua mpya inayoshajiisha usitishwaji mapigano na mazungumzo ya kuutatua mzozo huo.
Jeshi la Ethiopia linaonekana kuimarika kutokana na ndege zisizo rubani zilizonunuliwa China, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu, alisema William Davidson wa shirika la utatuzi wa migogoro la kimataifa (ICG).
"Vikosi vya Tigray vinaonekana vipo kwenye nafasi nguvu baada ya kuachia maeneo vilivyokuwa vikiyadhibiti," alisema.
Mapema wiki hii, mkuu wa vikosi vya Tigray alisema wapiganaji wake wamemriwa kujiondowa kwenye maeneo waliyokuwa wakiyashikilia na kurejea jimboni Tigray.
"Nimeviamuru vikosi vya Jeshi la Tigray ambavyo viko nje ya mipaka ya Tigray kuondoka na kurejea ndani ya mipaka ya Tigray mara moja," alisema Debretsion Gebremichael kwenye barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambayo pia ilipendekeza kuwepo kwa usitishaji mapigano mara moja utakaofuatiliwa na mazungumzo.
Vile vile, alipendekeza kuwepo kwa eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka ili kuzuwia mashambulizi kutoka angani kwenye mkoa wake na kuwekwa kwa vikwazo vya silaha dhidi ya Ethiopia na Eritrea.
Hasara ya vita vya mwaka mmoja
Makumi kwa maelfu ya watu wameuawa katika mzozo huo wa Tigray uliozuka mwezi Novemba 2020 kati ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na wapiganaji kutoka jimbo la Tigray, waliokuwa na nafasi za juu kwenye serikali ya Ethiopia kabla ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018.
Kutokana na mzingiro wa miezi kadhaa uliowekwa na wanajeshi wa serikali dhidi ya jimbo hilo, wakaazi wapatao milioni nane wa Tigray wameanza kufa njaa, kwa mujibu wa mashirika ya misaada.
Maelfu ya watu jamii ya Tigray wametiwa nguvuni ama kufukuzwa kwenye makaazi yao katika mazingira yaliyochochewa na kauli dhidi ya Watigray zinazotolewa na maafisa wa serikali, ambazo baadhi ya makundi ya haki za binaadamu yanasema ni kauli za chuki.
Mwezi uliopita, serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari wakati wapiganaji wa Tigray walipokuwa wakikaribia mji mkuu, Addis Ababa, na kutenda vitendo kadhaa vya udhalilishaji dhidi ya watu wa jamii ya Amhara, kwa mujibu wa wakaazi wa huko, huku vikosi vya Tigray vikisema vinapambana ili kuondosha mzingiro dhidi ya watu wao.