Afrika ya Kusini kupeleka wanajeshi 1,500 nchini Msumbiji
29 Julai 2021Bunge la Afrika ya Kusini limesema katika taarifa kuwa Rais Cyril Ramaphosa ameruhusu kupelekwa kwa wanajeshi wapatao 1500 nchini Msumbuji kwa lengo la kuisaidia nchi hiyo kupambana na vitendo vya ugaidi na wanamgambo wenye itikadi kali.
Mashambulizi yameongezeka nchini Msumbiji kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, na kuzusha hofu kuhusu mzozo huo kuenea kwenye nchi jirani.
Makundi ya wapiganaji wa itikadi kali yamekuwa yakifanya mashambulizi katika mkoa wa Cabo Delgado tangu mwaka 2017, na kusababisha vifo vya watu 3,100 na wengine laki nane kuyahama makazi yao kwa mujibu wa shirika la utafiti wa mizozo la ACLED.
Kikosi hicho cha wanajeshi kutoka Afrika ya Kusini kitasalia nchini Msumbiji kwa kipindi cha miezi mitatu, kufuatia makubaliano ya mwezi Juni ya Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC.
Operesheni hiyo ya wanajeshi wa Afrika kusini itagharimu dola milioni 66. Afrika Kusini ndio nchi ya hivi karibuni kupeleka wanajeshi wake baada ya Botswana kufanya hivyo mapema wiki hii na Rwanda ambayo iliwapeleka wanajeshi wake 1000 mwanzoni mwa mwezi huu.
Rwanda yakanusha madai ya kuhifadhi maslahi ya Ufaransa nchini Msumbiji
Akizungumza na wandishi habari hii leo, mjini Kigali, waziri wa rwanda wa mambo ya nje, Vincent Biruta ametetea hatua ya nchi yake kuwapeleka wanajeshi nchini Msumbiji.
''Ninachoweza kuwaambia ni hiki, kabla ya jeshi letu kutumwa kule ni serikali ya Msumbiji iliyokuja kutuomba kufanya hivyo siyo nchi nyingine yoyote. Na hili lilizingatia makubaliano yaliyokuwepo hapo kabla baina yetu kama nchi mbili kwenye nyanja mbalimbali ukiwemo usalama'',alisema Biruta.
Jumanne bunge la Angola lili idhinisha hatua ya kupelekwa kwa wanajeshi 20 wa nchi hiyo, kama sehemu ya kikosi cha jumuiya ya SADC nchini Msumbiji. Mwezi Juni, Jumuiya ya SADC iliidhinisha kupelekwa kwa kikosi cha wanajeshi wake ilikukabiliana na makundi ya itikadi kali katika eneo la kaskazini mwa msumbiji lenye utajiri wa gesi.
Mafanikio ya vikosi vya kimataifa
Jumapili Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji,ambaye kwa muda mrefu alikataa kupelekwa kwa vikosi vya nje nchini mwake, alipongeza juhudi za kijeshi za nchi za Kiafrika. Nyusi alisema vikosi vya kimataifa vitaunga mkono vile vya Msumbiji kurejesha amani na utulivu. Akiongeza kuwa nchi yake haitakiwi kuwa peke yake katika kupambana na ugaidi.
Moja ya mafanikio muhimu tangu kuwasili kwa wanajeshi wa Rwanda ni kudhibiti kituo cha polisi cha Awese,ambacho kilikuwa ngome ya wanamgambo kwa zaidi ya mwaka mmoja. Rais Nyusi alisema kuwa vikosi vya serikali vimedhibiti Awese, kijiji kidogo lakini muhimu karibu na mji wa Micimboa da Praia, ulio tekwa na wanamgambo Agosti mwaka jana.
Hata hivyo idadi kamili ya wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya SADC watakaopelekwa nchini Msumbiji haija fahamika. Umoja wa Ulaya pia ulitangaza kutuma ujumbe wa kijeshi nchini Msumbiji kutoa mafunzo ya kijeshi katika miezi kadhaa ijayo. Nusu ya wanajeshi hao watatokea Ureno ambayo ni mtawala wa zamani wa Msumbiji.