1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati Uganda wapinga washukiwa kuuawa

Lubega Emmanuel 23 Novemba 2021

Wanaharakati wa haki za bindamu, viongozi wa kidini  pamoja wanasiasa wamepinga vikali tamko la rais Yoweri Museveni wa Uganda kwamba vyombo vya usalama vina haki kuwaua watu wanaoshukiwa kuwa magaidi.

https://p.dw.com/p/43MMh
zur Nachricht - Überfall auf eine Militärkaserne in dem westugandsichen Bundibugyo
Picha: Reuters

Wanapendendekeza serikali ifanye mazungumzo na kundi la waasi wa ADF ambalo  linadaiwa kuleta hali ya sintofahamu si tu katika nchi jirani ya Congo lakini pia nchini Uganda wanakodaiwa kuhusika katika kuripua mabomu.

Katika kipindi cha miezi minne sasa watu wanaoshukiwa kuhusika katika ugaidi wameuawa na vyombo vya usalama nchini Uganda huku zaidi ya mia wakikamatwa bila kufikishwa mahakamani. Watu hao wanadaiwa kuwa wa kundi la Allied Democratic Front ADF , kundi la waasi kutoka Uganda ambalo hudaiwa kuendesha harakati zao kutoka ngome zao  Mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mauaji ya hivi majuzi ya sheikh mmoja ambaye familia yake wanasisitiza aliuawa akiwa amefungwa pingu baada ya kukamatwa yameibua tena mjadala kwa  nini washukiwa wauawe badala ya kufikishwa mahakamani. Rais Yoweri Museveni anasisitiza kuwa kile wasichafahamu wananchi, watu hao ni hatari na hujaribu kukabiliana na maafisa wa vyombo vya usalama pale wanapokamatwa na kwa hiyo kuwaua ndiyo hatua ya pekee ya maafisa hao kuhakikisha usalama wao.

Ugandan opposition leaders Robert Kyagulanyi and Kizza Besigye
Viongozi wa upinzani UgandaPicha: AFP/Getty Images

Lakini ufafanuzi wa rais Museveni umepingwa vikali na watetezi wa haki za binadamu , viongozi wa kidini na wanasiasa wa upinzani. Wanahoji kwa nini mshukiwa auawe bila kupitishwa katika mchakato wa kisheria na kwa hiyo ni rahisi mtu asiye na hatia kuua.

Tangu mapema miaka ya 2000, kundi la ADF limehusishwa na mashambulio kadhaa na mauaji ya raia hasa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Juhudi za kukomesha harakati za nchi hiyo zimelezewa kuhitaji ushirikiano wa Uganda na serikali ya Congo. Lakini haijafahamika kwa nini suala hilo limechelewa kushughulikiwa na pande zote mbili licha ya raia wa Congo kutoa kilio cha mashambulizi ya mara kwa mara. Sasa baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani nchini Uganda wanapendekeza serikali izingatie kuanzisha mazungumzo ya amani na waasi wa ADF. 

Chama cha Wanasheria wa Kiislamu nchini Uganda nacho kimetoa mwito kwa serikali kukomesha mauaji ya washukiwa wa  ugaidi . Kina mtazamo kuwa mwenendo wa kuwaua washukiwa utazidi kuleta mashaka kama kweli vyombo vya usalama vina nia ya kukomesha hali ya isntofahamu ya mashambulizi ya mabomu ikiwa hawana nia kufanya uchunguzi.Lubega Emmanuel DW Kampala