1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati sita wawekwa kizuizini Uturuki

Yusra Buwayhid
18 Julai 2017

Mahakama ya Uturuki leo imeamrisha wanahatakati sita ikiwa ni pamoja na mkurugenzi wa shirika la Amnesty International waendelee kuwekwa kizuizini kabla ya kufunguliwa mashtaka, kwa madai ya kusaidia kundi la kigaidi.

https://p.dw.com/p/2ghov
Amnesty International Protest Türkei Festnahmen
Picha: Getty Images/E.Dunand

Mkurugenzi wa tawi la Uturuki la shirika la Amnesty International Idil Eser alikamatwa Julai 5  na wanaharakati wengine saba pamoja na wakufunzi wawili wa kigeni wakati wa semina inayohusu usalama wa kidijitali na usimamizi wa habari katika kisiwa cha Buyukada, kilichopo kusini mwa mji wa Istanbul.

Mtafiti wa tawi la Uturuki la shirika la Amnesty Intrnational, Andrew Gardner ameliambia shirika la habari la AFP kwamba sita kati ya hao kumi wamebaki kizuizini na wanne wameachiliwa huru chini ya udhibiti wa mahakama, wamezuiliwa kusafiri nje ya nchi na wanatakiwa kuripoti kituo cha polisi mara kwa mara.

"Kwa kweli ni uhalifu wa kazi yetu yote tunayoifanya. Hiki si kitisho kwa watu hawa kumi pekee bali ni kitisho dhidi yetu sote, vuguvugu zimala wanaharakati wa nchini Uturuki. Ni siku ya giza sana kwa mfumo mzima wa haki wa Uturuki. Kwa mara nyingine tena inathibitishwa kwamba sheria haifuatwi nchini humu. Hii ni kesi ya kisiasa na ni onyo kwetu sisi sote kuwa hatuna usalama," amesema Andrew Gardner.

Kufungwa kwa wanaharakati hao kumezua wasiwasi duniani kote na kuongeza hofu ya kudidimia kwa uhuru wa kujieleza chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan.

Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya wanaharakati hao, ambao bado hawakuhukumiwa au kufunguliwa mashtaka rasmi, kuzungumza mbele ya waendesha mashataka kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwao.

Miongoni mwao ni raia wa kigeni

Wakufunzi wa kigeni - ambao mmoja ni raia wa Ujerumani na wa pili ni raia wa Uswisi  ambao walikuwa wakiongoza semina hiyo inayohusu usalama wa kidijitali, bado wamewekwa kizuizini kabla ya kufunguliwa mashataka yoyote.

Amnesty International gegen Türkei
Wanaharakati wakiwa wamebeba picha za waandishi habari waliowekwa kizuizini UturukiPicha: Getty Images/S.Gallup

Haikuwekwa wazi ni shirika gani la kigaidi wanaloshutumiwa kuliunga mkono lakini taarifa za vyombo vya habari vya Uturuki zimesema waendesha mashataka walioamrisha kukamatwa kwa wanaharakati hao, waliwasilisha rekodi za ushahidi wa mawasiliano yao na watuhumiwa wanaohusishwa na wapiganaji wa Kikurdi na wanamgambo wa siasa za mrengo wa kushoto pamoja na vuguvugu linaloongozwa na kiongozi wa kidini aliyepo uhamishoni nchini Marekani, Fethullah Gulen, anayeshutumiwa kupanga jaribio la mapindunzi la mwaka jana lililoshindwa.

Uturuki ilitangaza hali ya hatari siku kadhaa baada ya kutokea jaribio hilo la mapinduzi na kuanza kuchua hatua kali za kinidhamu dhidi ya watu wanaoshukiwa kuhusika na jaribio hilo lakini baadae wanasiasa, waandishi habari na wanaharakati pia walijumuishwa katika mchakato huo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/afp

Mhariri: Caro Robi