Wanachama wengi wa SPD wataunga mkono serikali ya mseto
3 Machi 2018Wahafidhina wanaoongozwa na kansela Angela Merkel,wataunda serikali pamoja na chama cha SPD lakini kiongozi huyo mwandamizi wa chama hicho ameonya kwamba kura ya "hapana" italeta maafa kwa chama hicho, Ujerumani na Ulaya kwa jumla.
Thomas Oppermann, makamu wa spika wa bunge la Ujerumani Bundestag, aliliambia gazeti la Die Welt kwamba anatarajia "uidhinishaji ulio wazi" kwa kiwango cha asilimia 55 katika kura ya chama cha SPD iliyopigwa kwa kutumia barua kupitia posta zoezi lililomalizika rasmi jana Ijumaa, ambapo matokeo yatapatikana kesho Jumapili.
Wanachama 464,000 wa SPD wanalazimika kupiga kura juu ya iwapo waidhinishe uamuzi wa viongozi wa chama chao kuendelea na kile kinachofahamika kama "muungano mkuu" na wahafidhina wanaoongozwa na kansela Angela Merkel ambao umeitawala nchi hiyo tangu mwaka 2013 licha ya kushindwa kwa kiasi kikubwa kwa chama cha SPD katika uchaguzi mkuu wa taifa mwezi Septemba.
Kukataa ushirikiano mwingine na vyama vya kihafidhina "kutakuwa ni maafa makubwa kwa Ujerumani, SPD na juu ya yote , kwa Ulaya," Oppermann alisema.
Tawi la vijana
Tawi la vijana la chama cha SPD limekuwa likipigia debe wanachama wake wapige kura ya hapana dhidi ya kurudiwa kwa muungano mkuu, likidai kwamba watakuwa bora zaidi kujijenga upya upande wa upinzani baada ya chama hicho kupata kipigo na kupata matokeo mabaya kabisa tangu mwaka 1993 katika uchaguzi wa mwezi Septemba.
Oppermann amewavulia kofia viongozi wa tawi la vijana kwa kuzusha mjadala mkubwa ndani ya chama, na kusema anatarajia kiongozi wao, Kevin Kuehnert, ataendelea kuweka ushawishi wake katika chama.
Amesema chama cha SPD kinahitaji "kujiamini zaidi", kuwa wajanja kidogo na kuwa tayari kwa mizozo" katika serikali ya muungano ijayo.
"Kitisho kikubwa zaidi kitakuwa kwamba tunarejelea kile tulichokifanya mara ya mwisho," amesema, akionya kwamba mtazamo wa kinyonge wa SPD unaweza kusababisha matokeo mabaya zaidi katika uchaguzi baada ya miaka minne.
Chama cha SPD awali kilipanga kubakia katika upinzani, lakini kilikubali kufanya majadiliano na wahafidhina wanaoongozwa na Merkel baada ya mazungumzo na chama kinachopendelea wafanyabiashara cha FDP na kile cha walinzi wa mazingira The Greens katika muungano wa vyama vitatu kuvunjika mwezi Novemba.
Kiongozi wa chama cha FDP Christian Lindner aliyaambia magazeti ya Funke Mediengruppe, kwamba uchaguzi mpya utakuwa suluhisho bora zaidi iwapo wanachama wa SPD watapiga kura ya "hapana". Ameondoa uwezekano wa kurejea tena muungano wa vyama vitatu, kutokana na misimamo ya vyama hivyo vinavyohusika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri : Jacob Safari