Urusi yawakamata 60 uvamizi wa uwanja wa ndege Dagestan
30 Oktoba 2023Taarifa ya kukamatwa watu hao imetolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Urusi ikiwa ni sehemu ya hatua kadhaa zinazochukuliwa tangu kutokea mkasa wa kuvamiwa uwanja wa ndege wa jimbo la Dagestan jana jioni.
Hiyo jana kundi kubwa la waandamanaji, wengi wakipaza sauti na kusema "Allah Akbar" yaani "Mungu Mkubwa" walivunja milango na vizuizi vya Uwanja wa Ndege wa Makhachkala na baadhi wakatimua mbio kuelekea njia ya kurukia ndege.
Inaaminika kundi hilo lilikuwa ni la watu wanaoiunga mkono Palestina na ambao wameghadhibishwa na vita vinavyoendelea mashariki ya kati baina ya Israel na Kundi la Hamas.
Iliarifiwa kuwa waandamanaji hao walikuwa wanawatafuta abiria wa Kiyahudi miongoni mwa abiria wengine waliowasili kwa ndege iliyotoka Israel.
Viongozi wa Dagestan wasema kilichotokea uwanja wa ndege kimevuka mpaka
Ndege hiyo ya kampuni ya Red Wings ilitokea Tel Aviv na ilisimama kwa muda hapo Dagestan kabla ya safari ya kuelekea Moscow.
Hakuna anayeweza kusema kwa hakika nini kingetokea iwapo waandamanaji hao wangefanikiwa kuwabaini na kuwazuia abiria wa kiyahudi.
Picha za mnato na mikanda ya video zilionesha makundi ya wanaume wengine wakisubiri nje ya uwanja wa ndege wakisimamisha pia magari. Mwandamanaji mmoja alibeba bango lililosomeka "Wauaji wa watoto hawana nafasi ndani ya Dagestan".
Jimbo hilo la kusini mwa Urusi linalofahamika rasmi kwa jina la Jamhuri ya Kirusi ya Dagestan lina idadi kubwa ya waislamu na viongozi wake mashuhuri wamekaririwa siku za karibuni wakitoa matamshi ya kuinguka mkono Palestina lakini vilevile wakikemea shambulizi la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la Hamas ndani ya ardhi ya Israel.
Ilichukua saa kadhaa kabla ya mamlaka za jimbo hilo kuchukua udhibiti kamili wa uwanja huo na kuwaondoa waandamanaji wote.
Gavana wa Dagestan Sergei Melikov ameapa kuwa wote waliohusika na kisa hicho wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema umma wa Dagestan unawahurumia Wapalestina na kuwaombea salama ili amani ipatikane, lakini vuramai iliyotokea uwanja wa Makhachkala ilivuka mpaka wa kuonesha mshikamano na Palestina.
Wizara ya Mambo ya Ndani imesema watu 150 waliohusika pakubwa na uvamizi wa uwanja wametambuliwa na kati yao 60 tayari wamekamatwa.
Israel yataka raia wake walindwe huku Marekani ikilaani kisa cha Dagestan
Kufuatia mkasa huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitoa mwito kwa mamlaka za Urusi kuwalinda raia wa Israel na jamii nzima ya Wayahudi na kuwashughulikia wote wanaochochea chuki dhidi yao.
Marekani ililaani kisa cha uwanja wa ndege wa Dagestan ikisema inasimama pamoja na jamii nzima ya kiyahudi katika wakati Washington inasema "chuki dhidi yao inaongezeka kote duniani"
Katika hatua nyingine Irani leo imeionya Marekani kujizuia kuilaumu Tehran na shambulizi la Hamas la Oktoba 7.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo Nasser Kanaani ametumia maneno mafupi tu ya kuitaka Marekani "iache maramoja" kuifungamanisha dola hiyo ya Uajemi na kile kilichofanywa na Kundi la Hamas.
Matamshi hayo yanafuatia kauli za viongozi wa Marekani ikiwemo rais Joe Biden kuashiria kwamba yumkini Iran inayo dhima fulani kwenye shambulizi hilo liliowauwa watu 1,400 na mamia wengine kuchukuliwa mateka.