Yaliyotokea hayasahauliki
27 Januari 2015Akihutubia bungeni mjini Berlin, Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Joachim Gauck amesema kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya Wayahudi yaliyotokea wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia Holocaust zinawahusu Wajerumani wote:
"Mtu hawezi kujitambulisha kuwa Mjerumani bila ya kujitambulisha na Auschwitz. Kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya Wayahudi, Holocaust, ni suala linalowahusu wananchi wote wa Ujerumani."amesisitiza rais Gauck.
Auschwitz ni onyo watu hawastahiki kutoa matamshi ya chuki dhidi ya wakibizi na wahamiaji
Kansela Angela Merkel kwa upande wake amewasihi Wajerumani wasisahau yaliyotokea na kusifu ile hali kwamba Wayahudi zaidi ya laki moja wanaishi humu nchini hivi sasa. Akikutana na watu walionusurika na kambi ya maangamizi ya Auschwitz, Kansela Merkel amesema "ni aibu kwamba watu nchini Ujerumani wanasumbuliwa, kutishwa au kushambuliwa wanapotamka kwamba wao ni Wayahudi au wanapoelemea upande wa taifa la Israel."
Kumbukumbu za mwaka huu zinafanyika katika wakati ambapo viongozi wa kisiasa nchini Ujerumani wanakabiliana na kishindo cha maandamano ya vuguvugu dhidi ya dini ya Kiislamu na dhidi ya wakimbizi na wageni. Katika hotuba yake, Kansela Merkel amesema Auschwitz ni onyo kwamba hawastahiki kutoa matamshi ya chuki dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.
Akizungumza mjini Paris kabla ya kuhudhuria kumbukumbu hizo za mauaji ya halaiki ya Wayahudi huko Auschwitz, Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesikitika kutokana na kuzidi kuongezeka hisia za chuki dhidi ya wayahudi na kusema hali hiyo haivumiliki.
Wafaransa 76 elfu wenye asili ya Kiyahudi walisafirishwa kwa nguvu - wengi wao hadi katika kambi ya maangamizi ya Auschwitz na kambi za kazi za sulubu wakati wa utawala wa Vichy uliokuwa ukishirikiana na Wanazi wa Ujerumani. "Ufaransa ni kwenu" amesema Rais Hollande mbele ya Wafaransa wenye asili ya Kiyahudi kufuatia ripoti wengi wao wanataka kuhamia Israel.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameroon pia ameshadidia umuhimu wa kukumbuka yaliyotokea katika vita vikuu vya pili vya dunia kama njia ya kupambana na ubaguzi.
Vladimir Putin atahadharisha dhidi ya minu ya kuiandika upya historia
Mbali na kumbukumbu zinazofanyika Poland, Umoja wa Mataifa pia unaikumbuka Januari 27- siku ya kukombolewa kambi ya maangamizi ya Auschwitz kwa kuandaa matukio kadhaa yatakayohudhuriwa miongoni mwa mengineyo na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon, na Rais Reuven Rivlin wa Israel. Hata hivyo kumbukmbu za Umoja wa mataifa zimebidi ziakhirishwe hadi kesho kutokana na theluji kali inayopiga mjini New York.
Naye Rais Vladimir Putin wa Urusi amepanga kuikumbuka siku ya kukombolewa kambi ya maangamizi ya Auschwitz kwa kulihutubia taifa hii leo. Rais Putin amesema "jaribio lolote la kuiandika upya historia au kuipotoa halitokubalika."
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP/
Mhariri: Mohammed Khelef