Walibya wataka mipasuko ikome na uchaguzi ufanyike
20 Juni 2024Umoja wa Mataifa unasema raia wa Libya wanataka mipasuko nchini mwao ikome na wanasiasa wanaohasimiana waandae uchaguzi.
Naibu mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya Stephanie Koury ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Walibya kutoka matabaka mbalimbali na maeneo yanayohasimiana wamechoshwa na migawanyiko inayoshuhudiwa nchini mwao na wanataka wadau wa siasa wautafutie ufumbuzi mkwamo wa muda mrefu na wakubaliane kuandaa uchaguzi wa kitaifa.
Soma pia: Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ajiuzulu
Koury ameliambia baraza la usalama amekuwa akikutana na viongozi wa siasa, wawakilishi wa mashirika ya kijamii, wasomi, makundi ya wanawake, viongozi wa kijeshi na wengine katika maeneo yanayohasimiana ya mashariki na magharibi kuwasikiliza maoni yao.
Amesema kuna makubaliano kwamba hali ya sasa haikubaliki na lazima ibadilike kuelekea uchaguzi na pande zote zitakuwa na wajibu wa kuyaheshimu matokeo.