1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliberia wapiga kura

10 Oktoba 2017

Wapiga kura watamchagua rais mpya atakayerithi urais kutoka kwa mwanamke wa kwanza kuwahi kushika nafasi hiyo Afrika Ellen Johnson Sirleaf mwenye umri wa miaka 72

https://p.dw.com/p/2lYgX
Liberia Monrovia Wahlen
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Vituo vya kupiga kura nchini Liberia  vimeshafunguliwa na wapiga kura wamejitokeza katika zoezi hilo muhimu kwa demokrasia ya nchi hiyo,katika wakati ambapo rais wa kwanza mwanamke barani Afrika anaondoka madarakani. Ellen Johnson Sirleaf ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 12.

Wapiga kura nchini Liberia wanaendelea na zoezi la upigaji kura lililoanza mapema leo asubuhi kumchagua rais mpya kati ya wagombea 20 wa kinyang'anyiro hicho.Uchaguzi huu unatarajiwa kuweka alama kwa mara ya kwanza tangu kipindi cha miaka 73 itakayoonesha kwamba rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia anayakabidhi madaraka kwa amani kwa atakayechaguliwa na wananchi kurithi kiti hicho.

Gambia Staatskrise ECOWAS Treffen  Ankunft Ellen Johnson
Rais anayeondoka-Ellen Johnson SirleafPicha: Reuters/A. Sotunde

Hadi sasa kuna wagombea watatu ambao wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Liberia wanaamini wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi. Kwanza ni  makamu wa rais Joseph Moakei wa chama cha mshikamano au Unity Party (UP) na wa pili ni aliyekuwa mchezaji soka maarufu wa Kimataifa George Weah ambaye anaongoza muungano mkuu wa upinzani  unaopigania Demokrasia ya mageuzi CDC na wa tatu akiwa ni Chales Brumskine kiongozi wa chama cha Liberty LP.

Agenda kuu zilizonadiwa na vyama hivyo katika kamepini za uchaguzi ni kuanzia kuimarisha uchumi,kuunda nafasi za ajira pamoja na kupambana na ufisadi na rushwa.Kila mgombea kati ya wagombea hao watatu anajinadi kwamba anakila sababu ya kuwafanya waliberia wamchague kuiongoza nchi hiyo,Charles Brumskine wa chama cha Liberty.

''Kuna vyama vikuu vitatu,chama cha Unity,CDC na UP sawa? kile walichowafanyia waliberia kitawarahisishia wananchi kufanya maamuzi yao.Wananchi watabidi kuchagua kati ya makamu wa rais aliyeshindwa,mcheza soka aliyefanikiwa na mwanasheria mwenye mafanikio.kwahivyo waliberia wanapaswa kuchagua kwa urahisi kabisa ni nani wanayemtaka aiongoze nchi hii kwa miaka sita ijayo''

Liberia bado imebakia kuwa  miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani na inaendelea kukabiliana na athari zilizojitokeza baada ya mgogoro wa maradhi ya Ebola yaliyozuka mwaka 2013 hadi 2015 ambapo kiasi watu 4000 wa nchi hiyo walifariki,bila ya kusahaulika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14.George Weah ni mgombea mwingine wa urais anayewekewa matumaini ya kushinda katika uchaguzi huu.

Liberia Wahlkampf
Picha: Reuters/T. Gouegnon

''Awali ya yote tutabidi kuunda serikali.Nchini Liberia bado tumegawika tunahitaji kuwaleta watu wetu pamoja,kutisha mkutano ili tuhimize mshikamano wa watu kuishi pamoja kwa amani na baade tutafute njia ya kuunda serikali itakayowashirikisha wote.Ili kila mmoja ajumuike na kufanya kazi kwa pamoja kuifanya nchi hii kuwa na mustakabali bora''

Rais anayeondoka madarakani Ellen Johnson Sirleaf ambaye anaangaliwa kama ni mwanamke shupavu ambaye pia ameshawahi kuwa mshindi mwenza wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 2011 katika hotuba yake jana Jumatatu aliwaambia waliberia kwamba hatma ya nchi yao iko mikoni mwao na hakuna anayemiliki kura zao sio kwa uwezo wa vyama,ukabila dini wala mafungamano ya kikabila.Matokeo ya rasmi ya mwanzo yanatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha saa 48 huku matokeo ya mwisho yakitarajiwa baada ya wiki mbili na   kimsingi endapo mgombea atakayepata asilimia 50 ya kura basi hapana shaka duru ya pili ya uchaguzi itaitishwa kati ya wagombea wawili watakaopata nafasi ya juu ambao watapambana katika kinyang'anyiro tarehe 7 Novemba.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW