Waliberia wamchagua rais
26 Desemba 2017Wagombea hao wawili walijiunga na wapiga kura wengine nchini Liberia leo wakati wakipambana katika uchaguzi huo wa rais ambao ulicheleweshwa wa duru ya pili.
Wapiga kura wanamchagua rais ambaye atachukua nafasi ya rais Ellen Johnson Sirleaf , ambaye atajiuzulu baada ya kutumia miaka 12 kaka rais wa kwanza mwanamke katika bara la Afrika , katika mabadilishano ya kwanza ya madaraka kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika magharibi tangu mwaka 1944.
Uchaguzi huo ulicheleweshwa kwa wiki saba kutokana na kufikishwa mahakama kwa malalamiko yaliyotolewa na chama cha Boakai cha Unity dhidi ya tume ya uchaguzi kuhusiana na uendeshaji wa uchaguzi wa duru ya kwanza.
Weah alikuwa nyota katika timu za kandanda barani Ulaya timu kama Paris Saint Germain na AC Milan katika miaka ya 1990 kabla ya kucheza kwa muda mfupi katika klabu ya Chelsea na manchester City nchini Uingereza mwishoni mwa muda wake wa kucheza kandanda.
Yee na Boakai walipiga kura katika vituo vya kupigia kura karibu na wanakoishi katika eneo la Paynesville, kitongoji cha mji wa Monrovia, mji mkuu wa taifa hilo lenye wakaazi milioni 4.6.
Kila mmoja atamba kuwa atashinda
Kila mmoja ametangaza kwamba ushindi ni wake katika kinyang'anyiro hicho. "Tutashinda ! Kwasababu watu wanatuamini na wanajua tunawakilisha kilicho bora," amesema Boakai , mfanyakazi wa umma kwa muda wa miongo minne, anayeonekana kwa mgombea wa serikali.
Lakini Weah pia nae alionesha matumaini kwamba kugombea kwa mara ya pili katika uchaguzi wa rais mara hii kutakuwa na mafanikio.
"Ushindi ni hakika , nina hakika kwamba nitashinda," aliwaambia waandishi habari baada ya kupiga kura yake.
Weah anadai kwamba udanganyifu katika uchaguzi ulimgharimu ushindi mwaka 2005 na makamu wa rais mwaka 2011. Chama chake cha CDC kilipinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 na 2011, lakini kimejizuwia hadi sasa kufanya hivyo mwaka huu.
Baada ya kupiga kura Jumanne (26.12.2017), Weah alionya kwamba "kile kilichotokea mwaka 2005 na 2011 hakiwezi kurejewa".
Boakai atoa onyo
Boakai pia alitoa onyo kama hilo, akisema atakubali matokeo iwapo tume ya taifa ya uchaguzi "itatimiza viwango vyote".
Boakai alipambana mahakamani kuhusiana na matatizo ya udhibiti wa foleni ya wapiga kura pamoja na utambulisho wa wapiga kura katika uchaguzi wa Oktoba 10 wa duru ya kwanza.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi Oktoba 10 , Weah alipata asilimia 38.4 ya kura wakati Boakai alikuwa wa pili akipata asilimia 28.8 ya kura. Hali hiyo ilisababisha kufanyika duru ya pili ya uchaguzi kwa kuwa hakuna mgombea aliyeweza kuvuka asilimia 50 ya kura inayohitajika kushinda uchaguzi moja kwa moja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isacc Gamba