Majimbo ya Ujerumani yadai fedha zaidi za wakimbizi
7 Mei 2023Wakuu wa majimbo ya Ujerumani wanaishinikiza serikali ya shirikisho kuhusu wasiwasi walionao juu ya gharama za kuwahifadhi wakimbizi. Viongozi wa majimbo nchini humo wamezidi kupaza sauti kuhusu wasiwasi wao Jumapili kabla ya mkutano wa wiki ijayo wa serikali ya shirikisho na wakuu wa majimbo ambao utazungumzia masuala yanayohusu gharama za uhamiaji. Miji ya Ujerumani imekuwa ikidai iongezewe fedha kwa ajili ya makazi na huduma kwa wakimbizi kwa hoja kuwa iko mstari wa mbele kuwahifadhi wakimbizi wapya wanaowasili hivyo inahitaji msaada zaidi wa kifedha. Ujerumani imekuwa kituo kikubwa cha wakimbizi wa Ukraine wanaokimbia uvamizi wa Urusi pamoja na waomba hifadhi kutoka mataifa ya Syria, Afghanistan na Iraq. Kwa mujibu wa ofisi ya uhamiaji na wakimbizi ya Ujerumani, hadi sasawaliotuma maombi ya kutafuta hifadhi ni karibu watu 100,000 tangu ulipoanza mwaka huu. Maombi 19,629 yaliwasilishwa katika kipindi cha mwezi Aprili peke yake.