1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
BiasharaUjerumani

Wakulima wauzuwia mji wa Berlin katika mgomo wa Trekta

19 Desemba 2023

Wakulima wa Ujerumani wameghadhabishwa na pendekezo la kupunguza ruzuku ya dizeli na ushuru unaowaathiri moja kwa moja, na unaoweza kuwagharimu hadi €1 bilioni. Serikali inasema hilo ni muhimu kusawazisha bajeti ya 2024.

https://p.dw.com/p/4aM1m
Ujerumani | Maandamano ya Wakulima Berlin
Wakulima wanapinga mpango wa serikali kuwaondolea ruzuku ya dizel na kuondoa punguzo la ushuru wa maschine za kilimo.Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Wakulima kutoka kote Ujerumani walishuka Berlin siku ya Jumatatu, na mamia ya matrekta yakikusanyika kwenye lango maarufu la Brandenburg la jiji chini ya kauli mbiu, "Too much is too much!"

Wakulima wamekasirishwa na uamuzi wa serikali ya shirikisho kufuta ruzuku ya mafuta ya dizeli pamoja na kukataa punguzo la ushuru kwenye ununuzi wa mashine za kilimo na misitu.

Kulingana na Chama cha Wakulima wa Ujerumani, mabadiliko hayo yanaweza kuwagharimu wakulima hadi euro bilioni 1 (takriban dola bilioni 1.1).

Serikali ya mseto imehalalisha hatua hiyo ikitaja haja ya kuziba pengo la Euro bilioni 17 katika bajeti ya nchi hiyo ya 2024, baada ya Mahakama ya Kikatiba ya Karlsruhe kuamua kuwa ni kinyume cha katiba kwa Berlin kutenga fedha ambazo awali zilitengwa kwa ajili ya msaada wa janga la corona kwa madhumuni mengine.

Soma pia: Kilimo bila Kemikali

Berlin inasema uamuzi wa mahakama ulifanya iwe muhimu kupunguza ruzuku zinazochangia kuharibu mazingira.

Ujerumani | Maandamano ya wakulima Berlin| Joachim Rukwied na Cem Özdemir
Waziri wa Lishe na Kilimo wa Ujerumani Cem Özdemir (kulia), na Joachim Rukwied, rais wa chama cha wakulima cha Ujerumani, wakizungumza wakati wa maandamano ya wakulima mjini Berlin, Desemba 18, 2023.Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Wakulima waahidi 'upinzani mkubwa'

Waziri wa Kilimo wa Chama cha Kijani Cem Özdemir alikuwa miongoni mwa waliokosoa mbinu ya serikali, akisema wakulima "hawana njia mbadala" kwa dizeli, akiongeza kuwa "wakulima ndio hutupatia chakula, upunguzaji huu unaiongeeza mzigo sekta hiyo."

Waziri wa Fedha Christian Lindner pamoja na Waziri wa Uchumi Robert Habeck wote wameonyesha nia ya kuwasikiliza wakulima lakini wanadai kuwa hawana nafasi kubwa kufanikisha hilo baada ya uamuzi wa Karlsruhe.

Wakulima sasa wanatafuta kutuma "ishara ya kwanza wazi" kwa muungano tawala wa vyama vitatu kwamba unahitaji kuacha upunguzaji uliopangwa.

Soma pia:Mpasuko waibuka ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu utoaji wa ruzuku ya kilimo 

Rais wa Chama cha Wakulima Joachim Rukwied alisema, "kama sivyo, kutakuwa na upinzani mkubwa kuanzia Januari. Hatutavumilia hili." Habeck alisema mtu yeyote anayetaka kubadilisha upunguzaji analazimika kuwasilisha njia zinazokubalika za kufadhili ruzuku hizo.

Ingawa mapato ya kilimo yamekuwa yakiongezeka, bei zinazoshuka za nafaka, mafuta na maziwa zimeanza kupungua faida.