Wakulima Poland wazuia barabara kuu mpakani mwa Ujerumani
25 Februari 2024Wakulima nchini Poland leo wamefunga barabara kuu iliyoko mashariki mwa mpaka na Ujerumani katika mgomo wa hivi karibuni dhidi ya kanuni na kodi za Umoja wa Ulaya. Mgomo huo ulianza saa saba mchana na kuzuia pande mbili za barabara.
Awali, wakulima hao walikuwa wamepanga kuizuia barabara hiyo kwa siku 25 lakini wamepunguza kufuatia mazungumzo baina ya wawakilishi wa ndani, wafanyabiashara na wasafirishaji.
Wakulima kote Ulaya, wamekuwa wakiandamana kwa majuma kadhaa, katika kile wanachodai ni sheria kali za mazingira, ushindani wa bidhaa za bei nafuu kutoka nje ya Umoja wa Ulaya na mapato duni.
Mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana mjini Brussels kesho Jumatatu. Watajadili mapendekezo mapya ya Tume ya Ulaya yanayolenga kubadilisha kanuni ambazo zimekuwa ndio kiini cha maandamano ya wakulima.