1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wateswa Uturuki

16 Desemba 2015

Kwa mujibu wa shirika linalopigania haki za binaadamu, Amnesty International, Uturuki imewashikilia kinyume cha sheria wakimbizi kadhaa wa Iraq na Syria na kuwashinikiza warejee katika maeneo ya vita.

https://p.dw.com/p/1HO3Y
Wakimbizi wa Syria na Afghanistan wakiwa wamekamatwa kwenye ufukwe nchini Uturuki wakijaribu kuingia kisiwa cha Lemnos cha Ugiriki.
Wakimbizi wa Syria na Afghanistan wakiwa wamekamatwa kwenye ufukwe nchini Uturuki wakijaribu kuingia kisiwa cha Lemnos cha Ugiriki.Picha: picture alliance/AA/B. Akay

Kwa mujibu wa shirika linalopigania haki za binaadamu-Amnesty International,Uturuki imewashikilia kinyume cha sheria dazeni ya wakimbizi na kuwashinikiza warejee katika maeneo ya vita.

Katika ripoti iliyopewa jina "Mlinzi wa lango la Ulaya",shirika la Amnesty International limesema maafisa wa serikali ya Uturuki wamewachukua wakimbizi na kuwatenga katika vituo maalum ambako hakuna aliyeweza kuwasiliana nao,na kuongeza kwamba kuna ripoti za watu kutendewa maovu ikiwa ni pamoja na kupigwa.

Uturuki inawapokea wakimbizi wasiopungua milioni mbili na laki mbili wa Syria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe viliporipuka mwaka 2011. Ingawa malaki wameelekea katika nchi za Ulaya,nchi hiyo bado inawahifadhi wakimbizi wengi zaidi kuliko nchi yoyote nyengine duniani.

Umoja wa ulaya na serikali ya Uturuki mjini Ankara wamefikia makubaliano mwezi uliopita yanayozungumzia kupatiwa Uturuki msaada wa dala bilioni tatu nukta mbili pamoja na nafuu nyenginezo ikiwa ni pamoja na kuruhusiwa waturuki kuingia bila ya viza katika nchi za Umoja wa Ulaya,ikiwa Uturuki itazuwia mikururo ya wahamiaji.

Amnesty Inatuhumu fedha za Umoja wa Ulaya zinatumiwa vibaya

Shirika la Amnesty International linasema limeorodhesha visa zaidi ya 100 vya wakimbizi waliohamishiwa kwa nguvu nchini Iraq na Syria na "linahofia idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi hivi sasa wakijumuishwa wale waliohamishiwa kwa nguvu nchini Afghanistan."

Ensaf Haidar Jahrestagung Amnesty International Deutschland 2015
Ensaf Haidar,mke wa mwanablogi Raif Badawi akihudhuria mkutano wa mwaka wa Amnesty International nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/A. Burgi

Afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Uturuki amekanusha dhana hizo na kusema ,idadi ndogo tu,ambayo haijafikia hata asili mia moja ya wakimbizi wa Syria ndio wanaokabiliwa na vizuwizi katika nyendo zao.

Ripoti ya shirka hilo la haki za binaadamu lenye makao yake makuu mjini London,inatuhumu kwamba baadhi ya fedha zilizotolewa na Umoja wa ulaya zinatumiwa kujenga vituo vya kuwashikilia wakimbizi ambako maovu yamegeuka kuwa jambo la kawaida.

"Inasikitisha kuona fedha za Umoja wa Ulaya zinatumiwa kugharamia mipango ya kushikiliwa watu kinyume cha sheria na kurejeshwa waliokotokea. Ripoti imesema , "Umoja wa Ulaya unabidi uhakikishe fedha inazotoa na ushirikiano wake pamoja na Uturuki vinainua na sio kuvunja haki za wakimbizi na wahamiaji."

Erdogan atuhumiwa kugeuka muimla

Wapinzani wa makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki walielezea tangu mwanzo wasiwasi wao kuhusiana na uvunjwaji wa haki za binaadamu nchini Uturuki. Nchi hiyo imeorodeshwa mstari wa chini kabisa wa faharasa ya uhuru wa vyombo vya habari na rais Recep Tayyip Erdogan amekuwa mara kwa mara akituhumiwa kugeuka muimla.

Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki,Recep Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri. Mohammed Abdul-rahman