1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Kongo wafukuzwa kutoka Angola

17 Oktoba 2018

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema raia wa Kongo wanaofukuzwa kutoka Angola wanarudi nchini mwao wakiwa katika hali ya kukata tamaa. Wengi wao walikuwa wanafanya kazi kwenye sekta ya madini.

https://p.dw.com/p/36g60
Uganda Flüchtlinge aus DR Kongo UNHCR Camp
Picha: Reuters/J. Akena

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Babar Baloch, raia wa Kongo wanalazimishwa kuvuka mpaka na kurudi nchini mwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kufukuzwa kutoka nchi jirani ya Angola. Karibu watu 200,000 wamewasili katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu wiki mbili zilizopita.

Idadi hiyo ya watu ni kutokana na uamuzi wa serikali ya Angola ya kuwafukuza wahamiaji wa Kongo, ambao wengi wao walikuwa wakifanya kazi katika sekta isiyo rasmi ya madini katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari huko Geneva, Uswisi, msemaji huyo amesema shirika hilo lina wasiwasi juu ya kuongezeka kwa haraka hali itakayosababisha mgogoro wa kibinadamu katika mkoa wa Kasai, ambako hali tayari ni tete.

Wakimbizi wa Kongo wakisubiri misaada inayotolewa na UNHCR
Wakimbizi wa Kongo wakisubiri misaada inayotolewa na UNHCRPicha: Michele Sibiloni/AFP/Getty Images

Msemaji huyo wa UNHCR amelezea pia juu ya msongamano wa watu katika mji wa Kamako ulio katika mkoa wa Kasai, kwenye mpaka wa Angola, amesema hali hiyo imefikia hadi watu wanalala nje, kwenye makazi ya familia nyingi zinazowakirimu, kwenye viwanja vya makanisa, na hata barabarani.

Katika baadhi ya maeneo ya Angola, kumekuwa na taarifa za mapigano na vurugu kati ya wahamiaji na mawakala wa utekelezaji wa zoezi hilo la kuwafukuza raia hao wa Kongo. Maelfu waliofika mpakani, wametoa malalamiko yanayojumuisha unyanyasaji wa kijinsia, kupigwa na kusababishiwa majeraha ya mwili na wizi wa mali mikononi mwa vikosi vya usalama kutoka pande zote za mpaka.

Bwana Baloch amesema kufukuzwa kwa watu hao ni kinyume na majukumu ya nchi chini ya mkataba wa Afrika juu ya haki za binadamu na kwamba shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linaziomba Angola na Kongo kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha usalama na watu wanavuka kutoka upande mmoja hadi mwingine kwa mpangilio maalum, pamoja na kuheshimu haki za binadamu na za wale walioathirika.

Mwandishi:Zainab Aziz/UN Press Release

Mhariri: Josephat Charo