Wakimbizi wa Iraq wanakabiliwa na mashaka
12 Agosti 2014Hussein Koban, mwanafunzi mjini Dortmund nchini Ujerumani, ameshindwa kulala kwa siku kadhaa kwa sababu familia yake, ambayo ni sehemu ya jamii ya Yazidi, ni miongoni mwa wakimbizi wapatao 1,000 wanaosubiri kuvuka mpaka wa Irak na Uturuki. "Nazungumza na jamaa zangu kila saa kwenye simu," alisema kijana huyo akionekana kabisa kuwa amekasirishwa na kukatishwa tamaa na hali ilivyo nchini Iraq.
"Wanasubiri kuruhusiwa kuingia Uturuki, lakini kwa sababu hawana vitambulisho hawaruhusiwi kuvuka mpaka. Hawana chochote cha kula. Watu hawa wamekata tamaa wanasubiri tu kuona kitakachotokea kutegemea majaliwa yao".
Kwa mujibu wa shirika la habari la Kikurdi, ANF, Wayazidi takriban 300 tayari wamewasili salama katika mji wa Silopi, nchini Uturuki.
Wayazidi wanahisi wamesalitiwa
Watu hao wa jamii ya Yazidi hawatafuti tu hifadhi nchini Uturuki, bali pia katika milima ya Sinjar katika eneo la mpakani na maeneo ya Wakurdi yanayopaka na Syria. Mwandishi wa habari wa Kikurdi, Barzan Iso, alilitembelea eneo la mpakani kati ya Syria na Iraq na kuzungumza na Wayazidi kadhaa. Kwenye mahojiano na DW, ripota huyo alisema wengi wao wanahisi walisalitiwa na vikosi vya Kikurdi vya peshmerga kaskazini mwa Iraq, ambavyo kimsingi vinatakiwa kulinda usalama katika eneo lenye utawala wake wa ndani la Kurdistan kaskazini mwa Iraq.
Wakimbizi wengi wanavishutumu vikosi vya Wakurdi kwa kuukimbia mji ya Sinjar ambao ni ngome ya Wayazidi na kuwaachia wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu la Iraq bila makabiliano yoyote. Mwanamke wa jamii hiyo amenukuliwa akisema wapiganaji wa kundi hilo waliingia mjini humo wakitumia magari manne na kwamba wapiganaji wa Kikurdi waliutoroka mji huo. Wayazidi wanahisi wameachwa na wamepoteza imani na wapiganaji hao.
Kwa mujibu wa Barzan Iso wapiganaji wa Kikurdi awali walikanusha madai yaliyotolewa dhidi yao lakini baadaye wakakiri walichagua mkakati usiofaa na kuwa makamanda waliokuwa na dhamana watawajibishwa ipasavyo.
Hali mjini Irbil inatisha
Wakati haya yakiarifiwa wakimbizi Wakristo na Wayazidi bado wamo mbioni kuyanusuru maisha yao. Wengi wao wamewasili katika mji wa Irbil, kaskazini mwa Iraq, ambako mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu kutoka Ujerumani, Fuad Zindani, mwenye nasaba ya Kikurdi, ameieleza hali kuwa ya kutisha.
Ameiambia DW kuwa "Wakristo na Wayazidi wamelazimika kujificha katika makanisa yaliyo karibu. Hawana chakula na mazingira ya usafi pole pole yameanza kugeuka kuwa janga."
Wakati wanamgambo wa Dola la Kiislamu walipolidhibiti eneo hilo waliwapa Wayazidi muda waondoke kutoka vijijini mwao katika kipindi cha masaa mawili au wasilimu. Watu waliingiwa na hofu na kwa haraka kukimbia. Inadaiwa wanawake kadhaa walibakwa na wanaume kadhaa kukatwa vichwa. Kwa mujibu wa walioshuhudia, Zindani alisema wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu waliwazuia watu walipokuwa wakikimbia na kuwalazimisha kutoa pesa na vitu vingine vya thamani. Alipokuwa akizungumza na DW kwa njia ya simu akiwa katika kanisa moja, kulitokea tafrani na muda mfupi baadaye mawasiliano yakakatika.
Eneo la kibinadamu kuingia Syria
Maelfu kadhaa ya Wayazidi wanatufa pia hifadhi katika eneo la Wakurdi lenye utawala wake wa ndani la Rojava nchini Syria, ambako kwa mujibu wa Barzan Iso, kundi la wapiganaji la Wakurdi la Syria, YPG, limetenga eneo salama la kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi.
Eneo hilo la kilometa 40 linaanzia katika mji wa Zakho nchini Iraq na huwaongoza wakimbizi hadi katika mji wa Al Yarubiyah, unaodhibitiwa na Wakurdi wa Syria. Mbali na kundi hilo, wapiganaji wa chama cha Wakurdi wa Uturuki, PKK, na wapiganaji wa Kikurdi wa peshmerga wanasaidia kulilinda eneo hilo. Iso amesema kufikia sasa zaidi ya Wayazidi 20,000 wamewasili nchini Syria kupitia njia hii.
Mwandishi: Josephat Charo/dw.de/english
Mhariri: Sekione Kitojo