Wakimbizi Afrika Magharibi, Kati wafikia milioni 14
20 Septemba 2024Kamishna Mkuu wa UNHCR kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Abdouraouf Gnon-Konde, amewaambia waandishi habari mjini Abidjan kuwa idadi hiyo imepanda kutoka wakimbizi milioni 6.5 mwaka 2019 hadi milioni 13.7 mwaka huu.
Gnon-Konde alisema kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idadi hiyo huenda ikaongezeka hadi kufikia kati ya watu milioni 14 na 15.
Soma zaidi: Afisa wa UN asema wanawake wakimbizi Sudan wanahitaji ulinzi
Hata hivyo, idadi hiyo haijumuishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako UNHCR inakadiria kuwa karibu watu milioni saba wamelazimika kuyahama makaazi yao.
Kutokana na kwamba watu wengi waliokimbia makaazi yao wanashindwa kurejea nyumbani kwa miongo kadhaa, UNHCR imezitaka nchi zinazowahifadhi kuwajumuisha wakimbizi katika mipango yao ya maendeleo.