1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajue viongozi wanaohudhuria mkutano wa G20

7 Julai 2017

Viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 wanakutana leo mjini Hamburg katika mkutano wa kilele. Viongozi 21 walialikwa kuhudhuria mkutano wa siku mbili.

https://p.dw.com/p/2g8Gi
Deutschland G20 Begrüßung der Teilnehmer durch Merkel
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Viongozi 19 wa nchi na serikali, pamoja na wawakilishi wawili kutoka Umoja wa Ulaya wanahudhuria mkutano huo, isipokuwa kiongozi mmoja tu ambaye ametangaza kutohudhuria.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel mwenyeji wa mkutano huo, ana nafasi nzuri na ushawishi mkubwa ndani ya nchi yake na kimataifa. Merkel ambaye anaonekana kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao wa mwezi Septemba kwa kipindi cha nne, mara nyingi huelezewa kama ''kiongozi wa ulimwengu huru,'' amesema tangu Marekani itangaze kujiondoa katika mkataba wa mazingira wa Paris, basi wasitarajie kuwa mazungumzo ya Hamburg yatakuwa rahisi.

Rais wa Marekani Donald Trump, anakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi nchini mwake, kuanzia mageuzi ya kodi hadi kashfa kuhusu madai ya kuwa na uhusiano na Urusi. Msimamo wake kuhusu sera yake kiuchumi na biashara ya kitaifa, pamoja na mtazamo wake wenye utata kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto duniani, huenda ikasababisha mivutano kwenye mkutano wa Hamburg.

Putin na Urusi kukutana ana kwa ana

Kiongozi mwingine anayehudhuria mkutano wa G20 ni Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana na Trump, litakuwa ni tukio muhimu zaidi katika mkutano huo wa kilele. Uhusiano kati ya Urusi na Marekani ni mbaya kwa zaidi ya miongo kadhaa. Putin ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika mizozo ya Syria, Ukraine na Korea Kaskazini.

Rais wa China Xi Jinping, ana nguvu zaidi kuliko watangulizi wake kama rais, kiongozi wa chama na mkuu wa jeshi. Hatua ya Trump kuifanya Marekani ijitenge, inaweza kumsaidia Xi kujionyesha mwenyewe kama mshirika muhimu katika biashara huria na mabadiliko ya tabia nchi, hata ingawa ukweli ni kwamba mtazamo wa China unaonekana tofauti.

Deutschland | G20 | Südkoreas Präsident Moon Jae-In, US-Präsident Donald Trump, Japans Premierminister Shinzo Abe
Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In (kushoto), Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe (Kulia)Picha: Reuters/C. Barria

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ana mamlaka zaidi kuliko hapo kabla, kutokana na ushindi alioupata mwanzoni mwa mwaka huu katika kura ya maoni ya kuifanyia mageuzi katiba. Ziara ya Erdogan nchini Ujerumani ambayo ni ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili ina utata kwa sababu ya mzozo uliopo katika uhusiano wa nchi hizo mbili. Serikali ya Ujerumani imemzuia Erdogan kuzungumza na Waturuki wanaoishi nchini Ujerumani.

Mfalme Salman wa Saudi Arabia, ni mmoja wa viongozi walioalikwa kuhudhuria mkutano huo wa Hamburg, lakini akatangaza kwamba hatohudhuria. Kwa mujibu wa ubalozi wa Saudi Arabia mjini Berlin, ujumbe wa Saudia utaongozwa na Waziri wa Serikali, Ibrahim al-Assaf.

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye ameahidi kufanya kazi pamoja na Merkel sio tu kwa ajili ya kuifufua Ufaransa, bali Umoja wa Ulaya kwa ujumla. Umoja wa Ulaya utawakilishwa na Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Rais wa Korea Kusini, Moon Jae In na Rais wa Argentina Mauricio Macri. Viongozi wengine ni Rais wa Mexico Enrique  Pena Nieto, Rais wa Brazil Michel Temer, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, Waziri Mkuu wa Australia Malcolm Turnbull, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pamoja na Rais wa Indonesia Joko Widodo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ DPA
Mhariri: Josephat Charo