Wajerumani wapiga kura
26 Septemba 2021Wajerumani leo 26.09.2021 wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wenye ushindani mkali kati ya vyama vikuu viwili,Social Democratic kinachoongozwa na Olaf Scholz na kile cha muungano wa kihafidhina cha Christian Democratic Union/Christian Social Union-CDU/CSU kikiongozwa na Armin Laschet.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu saa mbili asubuhi kwenye wilaya zote 299 za Ujerumani ambako wapiga kura leo watawachagua wabunge na chama wanachotaka kukipa mamlaka ya kumchagua Kansela mpya atakayeiongoza nchi hii katika makao makuu mjini Berlin.Mgombea wa chama cha SPD Olaf Scholz mara baada ya kupiga kura huko Aachen alitoa tamko hili.
" Leo ni siku nzuri na hali ya hewa inatoa ishara nzuri.Natumai kwamba raia wengi watajitokeza kupiga kura na kukufanikisha kinachotakiwa na hasa kukipa chama cha SPD ushindi mkubwa na raia kunipa jukumu la kuwa kansela Ajae wa Ujerumani-Nawatakia siku njema.
Rais wa shirikisho FrankWalter Steinmeier na mkewe nao pia wameshapiga kura mjini Berlin.Kuna wapiga kura walioamua kufika vituoni kupiga kura na kuna walioamua kupiga kura kwa njia ya barua ikiwemo Kansela Angela Merkel mwenyewe kutokana na janga la virusi vya Corona. Mpiga kura GUENTHER KESSLER,amesema
''Kila wakati ni muhimu kupiga kura ,lakini sasa ni muhimu zaidi na hasa kwakuwa kutakuwa na mabadiliko ya serikali.
Uchaguzi wa safari hii hapa Ujerumani ni mgumu kutabiri kabisa,ukitajwa kuwa mmoja ya chaguzi ambazo zimekuwa ngumu kutabirika katika kipindi cha historia ya hivi karibuni.
Kundi la muungano wa kihafidhina la Kansela Angela Merkel la CDU/CSU na chama cha wasoshalisti cha SPD viko kwenye mchuano mkali vikikaribiana kabisa katika uchaguzi huu kumrithi Kansela Merkel anayejiandaa kuliaga kabisa jukwaa la siasa baada ya kuiongoza nchi hii kwa miaka 16. Ni uchaguzi utakaoamua ni kina nani watakaoliunda bunge la 20 la Ujerumani tangu baada ya vita vya pili vya dunia na Kansela mpya atakayeanzisha ukurasa mwingine baada ya miaka 16 ya Kansela Merkel huku kukiwa na mashaka ya mwelekeo utakaochukuliwa.
Kura za maoni zinaonyesha kinyang'anyiro cha Ukansela kinaweza kuleta matokeo yafuatayo.Muungano wa kihafidhina wa vyama vya CDU-CSU utaambulia asilimia 23 kikitanguliwa kidogo na chama cha siasa za mrengo wa shoto cha Social Democratic SPD kitakachonyakua asilimia 25 ya kura,bila shaka hayo ni makadirio tu. Nico Siegel mkuu wa kampuni ya uchunguzi wa maoni ya wapiga kura ya Infratest Dimap anasema hapana shaka ni uchaguzi utakaoshuhudia baadhi ya maajabu.
Anasema licha ya SPD kuongoza kwenye kura ya maoni hadi dakika ya mwisho,huwezi kuondowa uwezekano wa ushindi kuelekea kundi la Wahafidhina la CDU-CSU.Kwa maneno mengine ngoma bado mbichi kwa pande zote mbili mpaka kipyenga cha mwisho kitakapopulizwa hapo matokeo ya mwisho yatakapotangazwa leo usiku.
Vituo vya kupigia kura vitafungwa rasmi saa 18.00 jioni. Ikumbukwe kwamba kiasi asilimia 40 ya wajerumani milioni 60 na laki 4 wenye haki ya kupiga kura bado hawajaonesha ni nani au chama gani watakichagua katika uchaguzi huu.Ikumbukwe tu kwamba mpambano wa kuwania kiti cha ukansela kwahakika ni kati ya waziri wa fedha wa sasa Olaf Scholz ambaye pia ni naibu Kansela,mwenye umri wa miaka 63 wa SPD na Armin Laschet,waziri kiongozi wa jimbo la North Rhine Westfalia na chaguo la Kansela Merkel kutoka muungano wa vyama ndugu CDU/CSU mwenye umri wa miaka 60.
Lakini yoyote atakayeshinda atategemea kuunda serikali ya mseto na chama cha Kijani kikipeperushiwa bendera na bibi Annalena Baerbock.Lakini tukumbushe tu kwamba vyama vyote hivyo vikuu viwili vikishindwa kupata wingi unaohitajika kuongoza peke yake basi inawezekana yakawepo mazungumzo ya muda mrefu,wiki kadhaa au hata miezi kutafuta maelewano ya kuunda serikali ya mseto.