1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisraeli waandamana kutaka mapigano yasitishwe Gaza

2 Mei 2024

Raia wa Israel wamemiminika mitaani kuitaka serikali kusitisha 'umwagaji damu' na kufikia makubaliano na Hamas ili kuwarejesha mateka, huku Colombia ikivunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel kupinga mauaji ya Gaza.

https://p.dw.com/p/4fQH5
Maandamano ya mateka Tel Aviv
Raia wa Israel wakiandamana kuishikiza serikali ya Benjamin Netanyahu kuwarejesha salama mateka waliosalia mikononi mwa kundi la Hamas kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Shannon Stapleton/REUTERS

Jamaa wa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na kundi la Hamas waliingia mitaani siku ya Alkhamis (Mei 2) kuishinikiza serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kundi hilo ili kurejeshwa kwa mateka wanaoshikiliwa na kwenye Ukanda wa Gaza. 

Katika mji mkuu, Tel Aviv, waandamanaji waliweka vizuizi kwenye barabara kuu nyakati za asubuhi, wakipiga mayowe ya kutaka makubaliano ya haraka ili kukomeshwa kile walichosema ni 'umwagaji damu' na kuwarejesha mateka wote nyumbani. 

Soma zaidi: Waziri wa mambo ya nje wa Marekani atembelea Gaza

Wengine walikusanyika mbelea ya nyumba ya Netanyahu kuwasilisha ujumbe wao. Mmoja wao alikuwa ni mama aliyebeba picha ya mtoto wake wa kiume, ambaye bado anashikiliwa mateka mikononi mwa Hamas

Mama huyo alisema yeye na familia yake wako kwenye hali mbaya sana kama walivyo maelfu ya raia wengine wa Israel. 

"Bado tuna mateka 133 ndani ya Gaza na tumekuja hapa mbele ya nyumba ya Waziri Mkuu Netanyahu asubuhi hii kumtaka na kumuambia na kumkumbusha kwamba macho ya wanawake wote, wanaume, mateka na raia wote wa Israel yanamuangalia yeye na baraza lake la mawaziri na tunamtaka afikie makubaliano, makubaliano muhimu ambayo yanatupa fursa ya kuwarejesha dada na kaka zetu nyumbani. Hatutasita kufanya hivyo hadi warejeshwe." Alisema mama huyo.

Hamas yataka ufafanuzi, Netanyahu atishia

Chanzo kimoja nchini Misri, kunakofanyika vikao vya kusaka mkataba wa kusitisha mapigano, kililiambia shirika la habari la AP kwamba viongozi wa Hamas walikuwa wamewaomba wapatanishi wa Misri na Qatar kutoa ufafanuzi wa kina wa pendekezo la Israel juu ya mkataba huo.

Tel Aviv Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken (kulia), akizugumza na baadhi ya jamaa watu waliotekwa na kundi la Hamas mjini Tel Aviv.Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Hamas walitaka kujuwa undani wa pendekezo la kuruhusiwa wakimbizi wa ndani kurejea kaskazini mwa Gaza bila masharti na kujiondowa moja kwa moja kwa wanajeshi wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa awamu ya pili.

Soma zaidi: Vita vya Gaza: Blinken akutana na Netanyahu

Lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, kwenye mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, siku ya Jumatano (Mei 1), Wazri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema serikali yake isingekubali kukomesha vita vyake vya Gaza kama sehemu ya makubaliano na Hamas.

Kwa mujibu wa ofisi yake, Netanyahu alisema pia kwamba hata makubaliano yagelipatikana, bado yasingelimaanisha kuepusha mashambulizi dhidi ya mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah.

Colombia yavunja uhusiano na Israel

Colombia ilitangaza kuvunja uhusiano wake na Israel kuanzia siku ya Alkhamis, baada ya Rais Gustavo Petro kuuelezea mzingiro wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kuwa ni sawa na mauaji ya kimbari.

Gustavo Petro Colombia
Rais Gustavo Petro wa Colombia ametangaza kuvunja uhusiano na Israel kutokana na mauaji yanayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Karen Toro/REUTERS

Uamuzi huu unafuatia ule wa kusitisha manunuzi ya silaha kutoka Israel na kuyalinganisha matendo ya taifa hilo kwenye Ukanda wa Gaza na yale ya utawala wa Kinazi nchini Ujerumani.

Soma zaidi: Netanyahu atishia kuishambulia Rafah

Kauli hiyo ya Rais Petro ilijibiwa haraka na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz, aliyeandika kupitia mtandao wa X kwamba "Historia itamkumbuka Gustavo Petro kwa kuamua kuegemea upande wa majitu makatili kabisa kuwahi kutokea ulimwenguni ambao waliwachoma moto watoto wachanga, wakawauwa watoto wadogo, kuwabaka wanawake na kuwateka nyara raia wasiokuwa na hatia."

Vyanzo: AP, Reuters