1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu DRC watakiwa kuwaombea wanajeshi mwezi wa Ramadhani

Jean Noël Ba-Mweze
11 Machi 2024

Jumuiya ya Kiislamu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (COMUCO) imewaomba Waislamu kuzidisha dua kwa ajili ya jeshi la nchi hiyo linalopambana na waasi upande wa mashariki wakati huu mfungo wa Ramadhani ukianza.

https://p.dw.com/p/4dNZ7
Wakimbizi mashariki mwa Kongo
Wanawake wakiuza na kununuwa kwenye eneo la mashariki ya Kongo wakati mwezi mtukufu wa Ramadhani ukianza.Picha: Edith Kimani/DW

Mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni kipindi cha mfungo kwa Waislamu na moja ya nguzo tano za dini hiyo yenye waumini wapatao bilioni mbili kote ulimwenguni ulianza siku ya Jumatatu (Machi 11).

Kuanza kwa mwezi huo kumesadifiana na kuendelea kwa mfungo wa Kwaresma wa jamii ya Wakristo, na wakati huo huo mapigano yakiendelea mkoani Kivu Kaskazini baina ya jeshi la Kongo na waasi wa M23.

Kutokana na hayo, Jumuiya ya Waislamu wa Kongo imetowa wito kwa waumini wa dini hiyo kuutumia mwezi huu wa kuomba toba na msamaha kwa kushirikiana na kusaidiana kwa mujibu wa sheria na maagizo ya dini yao. 

Wito huo ulitolewa katika siku hii ya kwanza ya mfungo huo ambapo Waislamu wa Kongo waliombwa pia kuongeza dua za kuliunga mkono  jeshi la taifa linalopambana na waasi wa M23 wanaoaminika kuungwa mkono na Rwanda mashariki mwa nchi hiyo.  

Waasi wa M23 mashariki mwa Kongo
Waasi wa M23 mashariki mwa Kongo.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/File/picture alliance

"Mwezi huu wa Ramadhani unajiri katika mazingira mahususi katika historia ya nchi yetu kufuatia mapigano yanayoendelea mashariki mwa nchi yetu ambapo hakuna shaka tena kuhusu ushirikiano wa kimataifa dhidi ya wakazi wa Kongo. Tunatoa wito wa kuimarisha maombi." Alisema Sheikh Ngongo Amani, mmoja wa viongozi wa jumuiya hiyo.

Wakristo watowa ujumbe wa amani mashariki mwa Kongo

Kwa upande mwengine, Wakristo nao wanaendelea na mfungo wa Kwaresma na maaskofu wa Kanisa la Katoliki Baraza la Kisangani walipaza sauti dhidi ya wavamizi na washirika wao wakiwemo baadhi ya viongozi wa eneo hilo.

Maaskofu hao walitoa wito pia kwa wabunge waliochaguliwa hivi karibuni watimize wajibu wao na waache kushirikiana na makundi yanayomiliki  silaha. 

Wakimbizi mashariki mwa Kongo
Makaazi ya wakimbizi wa mashariki mwa Kongo, ambako jeshi linapambana na waasi wa M23.Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

"Tumeshtushwa na unyonyaji hovyo pamoja na uporaji mkubwa wa maliasili zetu unaofanywa na wageni kwa ushirikiano na baadhi ya viongozi wetu. Tunaomba wabunge kupitisha sheria zinazokuza maendeleo ya wananchi, kudhibiti na kuwaadhibu viongozi wabaya, na kuacha kushirikiana na makundi yenye silaha." Alisisitiza Padri Archange Kambi, Katibu wa Baraza la Maaskofu la Kisangani. 

Maaskofu hao walivitaka vikundi vinavyomiliki silaha kuziweka chini na kutoendelea kuwaua Wakongo wenzao.

Hayo yamejiri huku ghasia zikiendelea katika eneo la Ituri na Kivu Kaskazini, mikoa miwili iliyo chini ya uongozi wa kijeshi lakini ambako makundi yanayomiliki silaha yanaendelea kuwahangaisha  raia.

Makundi hayo ni pamoja na ya wenyeji na yale ya kigeni. 

Imehaririwa na Mohammed Khelef