1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahuthi wanaendelea kuwa mwiba kwa Israel

1 Januari 2025

Kampeni kali ya kijeshi ya Israel dhidi ya washirika wa kikanda wa Iran imedhoofisha vibaya uwezo wake kuinyesha nguvu yake, lakini waasi wa Kihuthi wanasalia kuwa mwiba mchungu kwa Israel, wachambuzi wanasema

https://p.dw.com/p/4oiNj
Yemen Sanaa | Maandamano ya wafuasi wa Wahuthi
Wahuthi wameapa kuendelea na mashambulizi dhidi ya Israel hadi itakapoacha kuishambulia Gaza.Picha: MOHAMMED HUWAIS/AFP

Pamoja na makundi ya wapiganaji wa Kipalestina, Hamas na Hezbollah ya Lebanon, kudhoofika baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita, na kuanguka kwa Bashar al-Assad nchini Syria kuondoa kiungo muhimu katika "mhimili wa upinzani" wa Iran dhidi ya Israel, waasi wa Kihuthi wameibuka kuwa tishio la karibu zaidi kwa usalama wa Israel. 

Kundi hilo la waasi wa Kishia linalodhibiti sehemu kubwa ya Yemen, ikiwemo mji mkuu Sanaa, limeonyesha utayari wa kuishambulia mara kwa mara Israel kwa makombora na droni, licha ya kwamba lina uwezo mdogo wa kijeshi. 

Lakini eneo lao, lililoko umbali wa karibu kilomita 2,000, pamoja na athari zao za kusababisha machafuko—hususan katika njia muhimu za meli katika Bahari ya Shamu—unafanya kuwa vigumu kwa Israel kujibu mashambulizi ya Wahuthi, hasa ikiwa itachukua hatua peke yake, wanasema wachambuzi. 

Bahari ya Shamu | Mashambulizi ya Wahuthi dhidi ya meli ya mafuta
Mashambulizi ya Wahouthi yamevurugwa pakubwa usafiri wa meli katika Bahari ya Shamu.Picha: European Union's Operation Aspides via AP/picture alliance

Soma pia: Israel na Wahouthi washambuliana kwa makombora

"Kupambana na Wauthi ni kazi ngumu kwa Israel kwa sababu kadhaa, kubwa ikiwa ni umbali, ambao hauwezeshi mashambulizi ya mara kwa mara, na ukosefu wa ujasusi kuhusu kundi hilo," alisema Michael Horowitz, mkuu wa ujasusi wa Le Beck, kampuni ya ushauri wa kisiasa iliyoko Mashariki ya Kati, akizungumza na AFP. 

Msimamo wa Wahuthi na Wapalestina

Kama ilivyo kwa Hezbollah—ambayo ilianza kufanyiana mashambulizi ya mpakani na Israel baada ya shambulio la Hamas mnamo Oktoba 7 mwaka 2023 - Wahuthi wanasema wanachukua hatua kwa mshikamano na Wapalestina na wameapa kuendelea hadi kuwe na usitishaji wa mapigano katika Ukanda wa Gaza. 

Horowitz alisema anatarajia Israel kutumia mkakati sawa na ule wa kushughulikia Hezbollah, kwa kushambulia viongozi muhimu wa Wahuthi na kuvuruga njia za usafirishaji wa silaha kama ilivyofanya mara kwa mara nchini Lebanon na Syria. 

Hata hivyo, aliongeza, "Hakuna uhakika kuwa hili litarejesha vizuwizi." 

Ayatollah ataka Wahouthi kuungwa mkono

Athari kwa raia wa Israel

Licha ya kusababisha madhara madogo kutokana na mifumo ya juu ya ulinzi wa makombora ya Israel, mashambulizi ya kila siku ya Wahuthi katika wiki za hivi karibuni yamevuruga sana maisha ya raia nchini Israel. 

Soma pia: Netanyahu atoa oanyo kali kwa Wahouthi wa Yemen

Katika miji ya Jerusalem na Tel Aviv, ving'ora vya tahadhari vimekuwa vikilia mara kwa mara, na kuwalazimisha makumi ya maelfu ya wakazi kukimbilia kwenye makazi ya usalama, mara nyingi katikati ya usiku. 

Ingawa makombora na ndege nyingi zisizo na rubani zilizorushwa kutoka Yemen yanazuwiwa, kombora moja mwezi Desemba liliwajeruhi watu 16 huko Tel Aviv, kwa mujibu wa jeshi la Israel na idara ya huduma za dharura.

Katika kujibu mashambulizi hayo, jeshi la anga la Israel limefanya mashambulizi katika maeneo ya Wahuthi nchini Yemen, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa. 

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameapa kuwa Israel itakatilia mbali "mkono wa kigaidi wa mhimili wa uovu wa Iran," na Waziri wa Ulinzi Israel Katz ameapa "kuwasaka viongozi wote wa Wahuthi." 

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu | Ndege za kivita za Israel zashambulia bandari ya Hudaydah nchini Yemen.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kushoto, ameapa kukata kile alichokiita mkono wa mwisho wa "mhimili wa uovu" wa Iran. Picha: Israeli Prime Minister's Office/Anadolu/picture alliance

Mshirika muhimu wa Israel, Marekani, pia imefanya mashambulizi dhidi ya Wahuthi kuzuia mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu. 

Tathmini ya tishio

Mchambuzi Yoel Guzansky alikuwa na shaka kuhusu iwapo Israel itafanikiwa kuwadhibiti waasi wa Kihuthi. 

"Wahuthi wanasalia kuwa wa pekee wanaoendelea kushambulia Israel kila siku, na hili ni tatizo ambalo si rahisi kulitatua," alisema Guzansky, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Kitaifa katika Chuo Kikuu cha Tel Aviv. 

Soma pia: Israel yashambulia miundombinu ya Wahouthi Yemen

Hakuna "suluhisho la kimiujiza," aliongeza, kwa sababu nchi za Ghuba ya Kiarabu ambazo pia zimeathiriwa na mashambulizi ya Wahuthi "zinaogopa kuzuka kwa mgogoro mkubwa," jambo linaloifanya Israel kuwa makini inapojibu mashambulizi. 

"Wahuthi ni kero na tishio," alisema Menahem Merhavy, mtafiti katika Taasisi ya Truman katika Chuo Kikuu cha Kiebrania cha Jerusalem. 

Ingawa wanatoa "tishio dogo" kwa Israel, wamesababisha vurugu katika biashara ya baharini kwa kiwango cha kimataifa, alisema. 

Yemen | Maandamano wa wafuasi wa Wahuthi
Je, Israel na washirika wake wataweza kumaliza kitisho cha Wahuthi pia?Picha: AFP

Athari za kijiografia na makubaliano ya Abrahamu

Wakati wa muhula wake wa awali, Rais Mteule wa Marekani Donald Trump alisimamia makubaliano ya kihistoria ya urekebishaji uhusiano kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, na Morocco, yanayojulikana kwa pamoja kama Makubaliano ya Abrahamu. 

Tishio la kudumu la Wahuthi linamaanisha kuwa kuna "uwezekano mkubwa" wa uhusiano zaidi kati ya Waarabu na Israel, alisema Merhavy. 

"Iran imekuwa dhaifu sana na wazi kuwa ni hatarini kiasi kwamba ninaamini makubaliano kati ya Israel na Saudi Arabia yanaweza kutokea, hasa ikiwa kutakuwa na aina fulani ya usitishaji mapigano huko Gaza," alisema. 

Soma pia: Biden aahidi kuilinda Israel na vitisho vyote kutoka Iran

Mark Dubowitz, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya kifikra ya Foundation for Defense of Democracies yenye makao yake Washington, alionya kuwa Iran na washirika wake hawajashindwa kabisa. 

Tehran, alisema, "ina ujuzi wa kufufua mitandao yake ya washirika," na inaweza kuongeza kasi ya mpango wake wa nyuklia "kama hatua ya kujihami" dhidi ya Israel na Marekani.