Wahariri wasifu ziara ya Merkel Afghanistan
13 Machi 2012Mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" anatilia maanani kwamba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amewatembelea askari wa Ujerumani nchini Afghanistan licha ya mkasa huo. Mhariri huyo anaeleza kuwa ni hatari wakati wote kufanya ziara nchini Afghanistan. Lakini anasema ni muhimu kwamba Kansela Merkel ameifanya ziara hiyo, kwani vinginevyo dunia ingelipokea ishara kwamba hali ya Afghanistan haijadhibitika. Hata hivyo gazeti la"Mitteldeutsche Zeitung" linatilia maanani kuwa Kansela Merkel amekiri kwamba hali ya Afghanistan ni ngumu
Gazeti la "Hannoversche Allgemeine " linazitaka nchi za magharibi zijiulize kwa makini; nini kinaweza kutimizwa kwa uhakika, nchini Afghanistan hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2014 ?Mhariri wa gazeti hilo anasema baada ya kulipata jawabu linaloonyesha kwamba mambo hayaendi vizuri ,itakuwa sahihi kuanza kufanya mipango ya kuondoka. Watu wa Afghanistan ,anasema hawatapaswa kulalamika juu ya mipango hiyo. Sababu ni kwamba Waafghani wenyewe wanatoa mchango mdogo katika kuujenga mustakabal wa nchi yao.. Mhariri huyo amezitaka nchi za magharibi ziumalize mchezo wa patapotea zinaoucheza nchini Afghanistan .
Lakini mhariri wa "Westdeutsche Zeitung" anasema baada ya askari wa Marekani kuwaua raia 16,ni jambo la uhakika kwamba moto utawaka nchini Afghanistan. Kansela Merkel anayatambua hayo na ndiyo sababu hajatoa kauli ya uwazi juu ya terehe ya kuondolewa majeshi ya Ujerumani kutoka Afghanistan. Mhariri wa "Westdeutsche Zeitung" anaeleza kuwa Kansela Merkel hajaitamka wazi tarehe ya kuyaondoa majeshi ya Ujerumani kutoka Afghanistan.
Pia alirejea haraka kutoka Afghanistan baada ya kuyatembelea majeshi ya Ujerumani. Pana sababu mbili. Kwanza anatambua kwamba vita vya Afghanistan haviungwi mkono sana na Wajerumani. Jambo la pili ni kwamba Ujerumani siyo nchi yenye usemi mkubwa kwenye mfungamano wa nchi zilizochangia majeshi nchini Afghanistan. Wenye usemi mkubwa ni Wamarekani ambao hawafikirii kuurefusha muda wa uwepo wa majeshi yao katika vita ambavyo hawawezi kushinda.
Mhariri wa gazeti la "Donaukurier" anatoa maoni juu ya mgogoro wa nchini Syria. Anasema wakati wa kuleta mwafaka umeshapita nchini humo.Mhariri huyo anahoji kwamba ama Rais Assad aendelee kufanya ukatilii mpaka ashinde au atimuliwe. Hakuna njia nyingineLakini utawala wake unayumba. Kwa hivyo anasema mhariri wa Donaukurier " ikiwa jumuiya ya kimataifa itazungumza kwa kauli moja, njia ya Rais Assad itafikia mwisho haraka.
Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef