1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa kambi ya Mateso ya Auschwitz wakumbukwa

27 Januari 2006

Kwa miaka kumi sasa, tarehe 27 Januari hukumbukwa hapa Ujerumani kuwa ni siku ya kuwaomboleza watu waliokumbwa na mauaji ya kiholela, wahanga wa ukatili uliofanywa na utawala wa Ujerumani kabla na wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Novemba mwaka jana Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kwamba siku ambayo ilikombolewa kambi ya mateso ya Auschwitz hapo mwaka 1945 ikumbukwe duniani kote. Azimio hilo liliyataka mataifa yote yaikumbuke siku hiyo. Lakini umuhimu gani iliokuwa nayo suku hiyo hapa Ujerumani na duniani kote hii leo, ikiwa ni zaidi ya miaka 60 tangu kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia?

https://p.dw.com/p/CHnr
Mishumaa imewekwa katika Makumbusho ya Kambi ya Mateso ya Auschwitz
Mishumaa imewekwa katika Makumbusho ya Kambi ya Mateso ya AuschwitzPicha: AP

Ni miaka 61 sasa tangu kukombolewa kambi ya Mateso ya Auschwitz. Maiti za watu waliokufa, miili ya watu waliokondeana na kubakia mafupa tu ilikombolewa na majeshi ya Warussi kutoka kambi hiyo iliokuwa inasimamiwa na Wanazi. Picha za watu hao zilisambaa duniani na matokeo yake ni kwamba duniani kote kila mtu alikasirishwa na yale aliyoyaona na yaliotokea katika kambi hiyo.

Hadi leo picha hizo zinazoonesha ukatili uliotendeka katika kambi hiyo bado hazijapoteza umuhimu wake. Hata hivyo ilichukuwa miaka 50 hapa Ujerumani na miaka 60 duniani kote kuamuliwa kwamba kuweko na siku ya kuwakumbuka wahanga hao wa mauaji hayo ya kimbari. Kwanini imechukuwa muda mrefu kama huo? Mwanahistoria Profesa Nobert Frei wa kutoka Chuo Kikuu cha Jena ni mmoja kati ya mabingwa wanaoongoza katika historia ya karibuni:

+Hiyo inatokana sana kwamba maisha ya watu waliofanya ukatili huo wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia yanakaribia kumalizika, na ile hisia kwamba tokeo hilo halifai kusahauliwa imeongezeka zaidi katika miaka ya karibuni.+

Edna Brocke, mwenyewe Myahudi, na kiongozi wa jengo la zamani la Ibada la Wayahudi mjini Essen, hapa Ujerumani, anasema:

+Naamini kwamba jambo hilo la kuikumbuka siku hiyo halitokani na mauaji ya kiholela au na sisi Wyahudi, lakini linatokana na hali ilivyo hapa Ulaya. Ulaya, kwa mujibu wa fikra zangu, baada ya vita ilikuwa ni jamii iliosumbuliwa na kuathirika kimawazo, jamii iliokuwa katika mzozo katika kujipatia utambulisho wa kidini na pia wa kisiasa. Lakini nasikitika, kwa fikra zangu, ni kwamba mizozo hiyo haijatiliwa sana maanani.+

Suali la kimsingi ambalo pia linazushwa na wahakiki hapa Ujerumani ni nani hasa inayomsaidia kuikumbuka siku hiyo, wahanga wa mateso au jamii ya Kijerumani, na kwa namna gani?

Kuna watu wanaosema kwamba mauaji hayo ya kiholela yametokea wakati ambapo yasingeruhusiwa kutokea. Lakini yameshatokea, na lile suala kwamba mtu ayafanye mauaji hayo kama hayajatokea na hivyo kujaribu kutoyalipia fidia ni tatizo kwa Ulaya nzima.

Azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka wahanga wa mauaji ya kiholela ya Auschwitz wakumbukwe kila mwaka, siku kama ya leo, liliwasilishwa na Israel na likapitishwa pia kwa kura za nchi za Kiarabu na Kiislamu, kukiweko na mabadiliko kidogo. Katika mswaada kulitajwa pia kuengezeka hisia za kuwachukia Wayahudi, jambo ambalo linaonekana kote duniani. Sehemu hiyo ya mswaada haijapata uungaji mkono mkubwa katika Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, mtu anataraji kwamba siku hiyo ya kuwakumbuka wahanga wa Auschwitz italeta athari katika ngazi za kitaifa na pia za kimataifa.

Edna Brocke anahisi azimio hilo litaweza kuleta athari kwa vile limekubaliwa na Umoja wa Mataifa. Anadai kwamba katika miaka ya karibuni kumetokea watu zaidi wanaosema kwamba mauaji ya kimbari ya Auschwitz ni uongo, hayajatokea, na bila ya kutarajia ni kwamba hao wanaosema kuwa jambo hilo ni uongo ni wachache wanaotokea kambi ya kulia, lakini zaidi wanatokea katika vyombo vya propaganda vya dola, hasa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu. Rais wa Iran, Ahmadinedschad, hivi sasa anajulikana hapa Ulaya kutokana na msimamo huo, lakini Edna Brocke anasema msimamo huo umekuwa ukiwakilishwa katika nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa miongo ya miaka.

Bibi Brocke anasisitiza kwamba propganda hizo zinazoelemea upande wa serekali zimekuwa zikisambazwa kwa miaka.Pia ni kwamba kutokana na matangazo ya televisheni yanayorushwa kwa njia ya Satellite kutoka nchi za Kiarabu, propaganda hizo hupokelewa na Waislamu na Waarabu wanaoishi katika nchi za Ulaya, hivyo kusafirishwa hisia za kuwachukia Wayahudi hadi barani Ulaya, chukli ambazo watu wengi waliamini kwamba zimekiukwa hapa Ulaya baada ya kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Profesa Frei wa kutoka Chuo Kikuu cha Jena hana matumaini makubwa juu ya athari za siku hiyo ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa utawala wa Wanazi. Lakini matumiani yake yanajengeka kidogo kwa vile nchi nyingi za Kiislamu zinaiadhimisha siku hii ya leo.