Wahamiaji na kisa cha kuuliwa Khashoggi Magazetini
20 Novemba 2018Tunaanza na mkataba wa Umoja wa mataifa kuhusu wahamiaji ambao umezusha mdajala humu nchini mwezi chini ya mmoja kabla ya kuidhinishwa mjini Marakesh. Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linaandika: Ujerumani ni miongoni mwa mataifa 180 yaliyounga mkono mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wahamiaji. Mkataba huo uliofikiwa mwaka 2016 umepangwa kuidhinishwa decemba 11 na 12 inayokuja mjini Marrakesh nchini Moroko .Tangu kansela Merkel aliposema hatogombea tena wadhifa wa mwenyekiti wa chama chake cha CDU, kuna wanaojaribu kuitumia fursa hiyo kubadilisha mkondo wa siasa yake kuelekea wahamiaji. Chanzo ni kurejesha imani ya wapiga kura waliokimbilia upande wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD. Hiyo ni kazi bure .CDU wasitaraji watafanikiwa. Anaetaka kukishinda chama hicho anabidi mada moto moto kama hizo azishughulikie mapema na kwa njia za kuaminika."
Maovu hayawezi kuachiwa yapite hivi hivi
Ujerumani imekuwa nchi ya mwanzo miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya kuamua kusitisha biashara ya silaha pamoja na Saudi Arabia. Sababu zikio nyingi, kuanzia vita vya Yemen , kuvunjwa haki za binaadam hadi kufikia kisa cha kuuliwa mwandishi habari Jamal Khashoggi. Gazeti la Badische Zeitung linaandika: "Ni uamuzi wenye uzito mkubwa hasa kwa kuzingatia mchango wa Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Kweli, Saudi Arabia wanaweza kununua silaha kwengineko na ndio nafasi mia kadhaa za kazi zitahatarika nchini Ujerumani. Sawa pia kwamba siku za mbele watu hawatokwepa kuzungumza na dola hilo lenye nguvu katika kanda hiyo bila ya kujali nani anatawala. Hata hivyo uamuzi huo unastahiki, na ni onyo pia kwamba maovu hayaweza kuachiwa."
Wahafidhina wa Ulaya wapania kurejesha imani ya wapiga kura
Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika juhudi za mgombea wa chama cha wahafidhina wa Ulaya katika uchaguzi wa bunge la Ulaya utakaoitishwa mwakani-Manfred Weber. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika: "Mgombea mkuu wa chama cha wahafidhina wa Ulaya Manfred Werber anazitembelea nchi kadhaa. Hiyo si pekee ziara ya kupata imani ya wapiga kura mwanasiasa huyo wa kusini mwa Ujerumani, bali pai ya kuondowa dhana mbaya dhidi ya Ujerumani. Pindi akifanikiwa kuchaguliwa kama mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Ulaya , baada ya uchaguzi wa bunge la ulaya mwezi May mwakani, itakuwa fursa pia ya kuanzisha mageuzi ya kina na kuujongeza Umoja wa ulaya karibu zaidi na raia na kwa namna hiyo kuwapokonya hoja wale wanaoukosoa Umoja huo."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman