Wahamiaji kurejeshwa makwao kutoka Ujerumani
29 Desemba 2016Tukianza na mada kuhusu kurejeshwa kwa wahamiaji ambao maombi yao ya kubakia nchini Ujerumani yamekataliwa , gazeti la Leipziger Volkszeitung linaandika:
Haijawahi kutokea , ukamnunulia mtu tiketi ya ndege , na kumpa kiasi fulani cha euro na ukatarajia kuonana nae tena. Matumaini haya yanaweza kuwa ni ya kufikirika tu, wakati nchi anayokwenda mtu huyo kijiografia iko karibu tu na nchi yako. Kugharamia safari ya kurejea inawezekana pia kuwa safari ya kurejea, yaani huondoi uwezekano wa mtu huyo kurejea tena. Ndio sababu kwa wakati fulani ulazima wa kurejeshwa kwa watu kutoka katika mataifa ya eneo la Balkan magharibi muda wake umepunguzwa mno.
Ukweli ni kwamba : Utaratibu wa kugharamia safari ya kurejeshwa nyumbani haipaswi kuwa mtindo wa kuendelezwa, anasema hivyo mhariri wa gazeti la Braunschweiger Zeitung.
Sababu ni kwamba maombi ya hifadhi yana ncha nyingi. Ndio sababu ni sahihi pia , kuyaangalia kwa kutumia vitendea kazi tofauti kutokana na sababu zinazotofautiana katika kuomba ukimbizi. Wengi miongoni mwao , ambao hadi hii leo wanaishi nchini Ujerumani , walikuja kama wakimbizi , kwasababu katika mataifa ya eneo la Balkan kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, kutokana na sababu ya asili yao ama wanakandamizwa kutokana na dini yao.
Katika mada kuhusu mvutano kati ya Marekani na Israel baada ya baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kupiga kura katika azimio linaloitaka Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina, gazeti la Der Neue Tag linaandika.
Walowezi karibu 400,000 wa kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina inayokaliwa kimabavu na Israel ya magharibi mwa Jordan na walowezi 200,000 katika eneo la mashariki la Jerusalem ni ushahidi tosha , kwamba Netanyahu ana lengo moja tu , kuzuwia taifa la Palestina kuwapo na kuzuwia sera ya mataifa mawili kuishi pamoja. Kwa kuingia madarakani kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump , ambae Israel inatarajia kupata uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa , amani katika mzozo wa mashariki ya kati haitawezekana kabisa.
Tatu Gazeti la Donaukurier la mjini Ingolstadt linaandika kuhusu mpango wa kusitisha mapigano nchini Syria. Mhariri anandika.
Kwa wakati huu Vladimir Putin ameweza kwa ukamilifu kutumia mbinu ya kuwapo ombwe la madaraka katika Ikulu ya Marekani ya White House. Ameweza kuchukua fursa hiyo , kama anavyofanya kwa nchi yake Urusi, Iran na Uturuki kuhakikisha anaamua hali ya baadaye ya Syria , bila ya kupata upinzani kutoka Marekani. Pamoja na hayo lakini Putin ataihitaji hivi karibuni Marekani. Kuna maslahi makubwa yanayoambatana na mzozo wa Syria , kama vile Urusi kuleta uthabiti katika nchi hiyo peke yake.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inslandpresse
Mhariri: Grace Patricia Kabogo