1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina Ujerumani washindwa kuafikiana mgombea ukansela

19 Aprili 2021

Vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU nchini Ujerumani vimeshindwa kufikia makubaliano ya mtu atakayechukuwa nafasi ya Kansela Angela Merkel, baada ya muda wa mwisho vilivyojiwekea kumalizika usiku wa Jumapili.

https://p.dw.com/p/3sChd
Kombobild Armin Laschet und Markus Söder

Muda wa mwisho uliowekwa ilikuwa usiku wa Jumapili (Aprili 18) lakini ilipita bila ya muafaka baina ya chama cha Kansela Merkel cha CDU na mshirika wake CSU cha Bavaria, ambavyo vimekuwa kwenye mvutano mkali wa kuamuwa mgombea wa kiti cha ukansela kwenye uchaguzi huo wa baadaye mwaka huu. 

Wajumbe wenye nguvu kwenye vyama hivyo walikuwa wanawashinikiza wagombea wawili wakuu kumaliza tafauti zao, wakikhofia kwamba mpasuko baina yao unaweza kuhujumu uwezekano wa kurejea madarakani kwa muhula wa tano mfululizo katika uchaguzi wa Septemba. 

Armin Laschet, kiongozi wa sasa wa CDU na waziri mkuu wa jimbo lenye watu wengi la Northrhine Westphalia, na Markus Soeder, mkuu wa CSU na pia waziri mkuu wa jimbo lenye utajiri mkubwa la Bavaria, ndio vinara wa mkwamo huo. 

Wagombea hao na timu zao wamekuwa wakifanya mazungumzo kwa wiki nzima sasa kwa lengo la kuumaliza mkwamo huo kufikia jana, Jumapili. 

Mkwamo haujatatuka

Deutschland, Berlin | Armin Laschet, CDU-Präsidiumssitzung
Armin Laschet, waziri mkuu wa Northrhine-Westphalia na mwenyekiti wa CDU.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Lakini, licha ya pande zote mbili kuyaelezea mazungumzo yao kuwa mazuri, hakuna upande uliokubali kujiondowa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Soeder na Laschet walikutana kwenye jengo la bunge, Bundestag, mjini Berlin jioni ya Jumapili na wakatumia zaidi ya masaa matatu bila ya kufikia makubaliano, kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani (dpa).

Hata hivyo, hakuna upande uliokuwa tayari kuzungumzia waziwazi mkwamo huo, ambapo endapo ungeliendelea hadi jioni ya Jumatatu, basi ilibidi kesho yake upelekwe na kuamuliwa na kambi ya vyama hivyo bungeni. 

Kiasili, CDU na CSU huwa na mgombea mmoja wa nafasi ya ukansela, ambapo katika hali ya kawaida, mgombea kutoka CDU - ambacho ndicho chenye nguvu zaidi - ndiye mwenye nafasi ya kusimama kwa niaba ya vyama hivyo ndugu.

Walinzi wa Mazingira wajipanga kwa ukansela

Bundesdelegiertenkonferenz Bündnis 90/Die Grünen | Habeck & Baerbock, Bundesvorsitzende
Wenyeviti wenza wa chama cha Walinzi wa Mazingira (Die Grüne), Robert Habeck (kushoto) na Annalena Baerbock ambao wanawania kukiwakilisha chama chao kwenye uchaguzi wa ukansela wa Ujerumani.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Lakini uungwaji kwa chama hicho umekuwa ukishuka kwenye kura za maoni, katika wakati serikali ya Merkel ikipambana kulidhibiti janga la virusi vya corona, hali ambayo inamuweka Soeder wa CSU kwenye nafasi nzuri zaidi.

Hayo yakijiri, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia yake, chama cha walinzi wa mazingira (Die Grüne) kilitarajiwa kumtaja mgombea wake wa nafasi ya kansela siku ya Jumatatu (Aprili 19).

Robert Habeck na Annalena Baerbock, ambao wamekuwa wenyeviti wenza wa chama hicho tangu mwaka 2018, chama hicho kiliporejea tena kwenye uso wa siasa, ndio wanaowania nafasi hiyo. 

Kwa sasa, walinzi hao wa mazingira wako nyuma ya muungano wa CDU/CSU na mbele ya SPD - mshirika mdogo kwenye serikali ya mseto ya Ujerumani - kwenye kura za maoni.