Wagombea wa urais Uganda wazindua ilani zao
4 Novemba 2020Hao ni wafuasi wa Rais Yoweri Museveni alipokuwa akizindua ilani yake ya uchaguzi, ambapo anawania kiti cha urais kwa mara ya sita. Kipindi cha uchaguzi ni msimu mwingine tena kwa wanasiasa kutoa ahadi kwa Waganda kuhusu mikakati waliyonayo kuimarisha maisha yao kwa mujibu wa ilani zao za uchaguzi.
Rais Museveni amefafanua kuwa atazidi kulitanguliza suala la usalama wa nchi ili kuwawezesha wananchi na wawekezaji kuendesha shughuli zao katika mazingira yenye uhakika. Hii ni chini ya kaulimbiu yake ya kuihakikishia Uganda mustakabali mwema.
Soma pia:Bobi Wine aidhinishwa kugombea urais Uganda
Hata hivyo, wakosoaji wa Rais Museveni miongoni mwao wakiwa wagombea kiti hicho wamelezea ilani yake kuwa ni ile ile ambayo ameitumia kutawala Uganda kwa miaka 35 bila kuleta mageuzi thabiti ya kidemokrasia. Wanaelezea kuwa badala ya yeye kuwekeza katika masuala ya usalama ikionekana kuwa jeshi analotegemea kuendelea kumuweka madarakani, angeyapa kipaumbele masuala nyeti ambayo yanatoa fursa sawa kwa kila mwananchi kuboresha maisha yake. Mpinzani mkuu wa Rais Museveni, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anaeleza zaidi.
Wagombea wengine kwa tiketi ya vyama vikuu vya upinzani nao wameapa kuzirejesha taasisi za kiuchumi na kijamii zilizotupiliwa mbali na utawala wa Rais Museveni. Miongoni mwa hizo ni uchukuzi wa reli, mashirika ya wakulima pamoja na benki. Mgombea wa chama kikongwe cha DP Norbert Mao ambaye kaulimbiu yake ni kurudisha mustakabali wa Uganda amesema…
Mwanamke pekee anayegombea urais nchini Uganda, Nancy Kalembe ameelezea kuwa atatanguliza mbele maslahi ya wanawake. Anaamini kuwa maisha ya wanawake yakiimarika kutokana na wao kushiriki moja kwa moja katika masuala nyeti ya uongozi na uchumi, basi taifa litanufaika kuanzia ngazi ya familia. Kwa upande wao, wachungaji wawili ambao wanagombea urais wametamka kuwa watategemea zaidi sala kwa Mungu kuikomboa Uganda kiuchumi. Lubega Emmanuel DW, Kampala.
Lubega Emmanuel, Mwandishi wa DW, Kampala