Wagombea urais Kongo watoa ahadi tele kuelekea uchaguzi mkuu
19 Desemba 2023Ikiwa imesalia siku moja tu kwa uchaguzi huo kufanyika, tayari wagombea kadhaa wa urais wamejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho na kuwaacha wagombea 18 akiwemo rais wa sasa Felix Tshisekedi wakiwania nafasi hiyo ya juu.
Raia milioni 44 wa Kongo wamejiandikisha kama wapiga kura katika uchaguzi wa kesho wa urais, bunge na udiwani.
Soma pia: Tshisekedi: Uchaguzi wa Jumatano utafanyika katika mazingira ya kuaminika
Mbali na kunadi sera zao, wagombea hao walichukua muda mwingi kutupiana lawama na hata kauli nzito. Lakini miongoni mwa masuala yaliopewa kipau mbele ni suala la usalama.
Wagombea wote wa urais wameahidi kumaliza vita na machafuko ya muda mrefu eneo la mashariki mwa Kongo.
Fayulu: Nikichaguliwa rais nitavunja uhusiano na Rwanda
Rais Felix Tshisekedi amesema iwapo atachaguliwa kwa muhula wa pili ataliimarisha jeshi la nchi hiyo wakati Moise Katumbi akiahidi kuongeza mara dufu idadi ya wanajeshi na kupandisha mishahara yao.
Kwa upande wake, Martin Fayulu ameeleza kuwa, atavunja uhusiano wa kidiplomasia na nchi jirani ya Rwanda endapo atachaguliwa kuwa rais huku Denis Mukwege akiahidi kubadili mfumo mzima wa usalama.
Soma pia: Matamshi ya Cornelle Nangaa yaibuwa malumbano kati ya Kenya na DRC
Rais Tshisekedi amewashambulia hasa wapinzani wake na kuwaita kuwa ni wagombea wa nchi na maslahi za nje wakati wapinzani wake wakimkosoa kwa kushindwa kurejesha usalama na kuboresha mishahara ya wafanyakazi wa umma.
Wagombea wa upinzani pia wameikosoa tume ya uchaguzi CENI ambayo wamesema haijaweka wazi mchakato mzima wa uchaguzi.
Chama pekee ambacho hakikushiriki uchaguzi huo ni kile cha PPRD, chake rais wa zamani wa taifa hilo Joseph Kabila.