Wagombea kutoka pande zote
Wakati uchaguzi mkuu wa Ujerumani ukikaribia, wagombea wa ukansela wanataka kujionyesha tu katika mwanga bora. Mbali na sura yao ya kazi, wana sura nyingine isiyofahamika.
Nani atakuwa Kansela?
Hata kama ni vyama vya CDU na SPD tu vinavyoamini kwamba vinaweza kuwa na kansela katika uchaguzi wa Septemba, vyama vikuu vingine navyo vimesimamisha wagombea. Wagombea hao wanaviwakilisha vyama vyao katika kampeni. DW inawatambulisha wagombea hao na inaonyesha sura zao rasmi na upande wao mwingine wa kibinafsi.
Katika kilele cha madaraka
Kwa miaka minane sasa, Angela Merkel (59) amekuwa akiiongoza Ujerumani. Shughuli zake za kisiasa zilianza mwaka 1989 kwenye moja ya vyama vya kwanza vya kidemokrasia katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki na baadaye alihamia chama cha CDU. Akiwa Kansela, Merkel alibadili baadhi ya misingi ya chama chake: Aliondoa sharti la vijana kwenda jeshini na kuamua Ujerumani ipunguze nguvu za nyuklia.
Kutembea, kupika, kutawala
Anapokuwa na muda wa kupumzika, Merkel anapenda kutembea nje. Anapendelea zaidi kupanda milima na mume wake na kupika. Merkel alikulia katika iliyokuwa Ujerumani ya Mashariki. Huko alisomea Fizikia katika chuo kikuu. Merkel anaeleza, "Daima nilikuwa nikipenda masomo ya sayansi kwa sababu utawala wa Ujerumani ya Mashariki haukuweza kuingilia kanuni za kisayansi."
Mpinzani mkuu
Peer Steinbrück (66), mgombea wa chama cha SPD, amesema kamwe hatakaa aunde serikali na Angela Merkel. Kati ya mwaka 2005 na 2009 alikuwa waziri wa fedha katika serikali ya mseto ya SPD na CDU. Kwenye kampeni yake Steinbrück ametaka pawe na kiwango cha chini cha mshahara kilichowekwa kisheria na kiwango cha juu cha kodi za nyumba. Amekuwa akiiendesha kampeni yake kwa kejeli na kauli za uchokozi.
Mwenye mkakati
Kuanzia akiwa na miaka sita, Steinbrück amekuwa akicheza mchezo wa chesi. Anapenda kupambana na mabingwa wa dunia na wakati mwingine anacheza mchezo huo katika kompyuta. Steinbrück amewahi kuuelezea mchezo huo kama mchezo ambapo unaweza tu kujaribu kuwa bora kuliko mpinzani wako. "Lakini ninapocheza na kompyuta, sina nafasi ya kushinda."
Viongozi wawili wasioendana
Kila mtu anatakiwa kuhisi anawakilishwa na wagombea wawili wa chama cha walinda mazingira "Die Grünen". Katrin Göring-Eckardt (47) na Jürgen Trittin (59). Göring-Eckardt anatokea Mashariki huku Trittin akitokea Magharibi. Wote wanataka watu wenye kipato cha ju walipe kodi kubwa zaidi na wote walichaguliwa na chama chao katika uchaguzi wa moja kwa moja. Ni mara ya kwanza kwa jambo hilo kutokea.
Daima anashiriki
Jürgen Trittin hajali kwamba ameloa katika mto huu. Amezowea hali tete katika maandamano alipokuwa waziri wa mazingira. Trittin anapenda kuonekana katika maandamano ya kudai ulinzi zaidi wa mazingira au kupinga ubaguzi wa rangi. Hata hivyo, mwanasoshiolojia huyo hapendi kuzungumza juu ya maisha yake binafsi.
Anapenda kucheza dansi
Katrin Göring-Eckardt alijifunza kucheza dansi katika shule ya dansi iliyokuwa ikiendeshwa na baba yake. Amewahi pia kushiriki katika mashindano ya dansi. Ameeleza kuwa tangu wakati huo haogopi tena kuzungumza mbele ya umati wa watu. Ili kujikita zaidi katika kampeni, mama huyo mwenye watoto wawili ameweka chini wadhifa wake wa kuwa mwenyekiti wa mkutano mkuu wa makanisa ya kiinjili ya Ujerumani.
Uchumi, Fedha, Brüderle
Rainer Brüderle, mgombea wa chama cha waliberali cha FDP, mwanasiasa wa kiuchumi kwa asilimia mia moja. Daima amekuwa akishughulikia masuala ya uchumi - tangu alipoanza kufanya kazi ya siasa huko Mainz hadi alipoteuliwa kuwa waziri wa uchumi chini ya Merkel. Baada ya chama chake kupoteza kura nyingi katika chaguzi za majimbo, Brüderle alijiuzulu mwaka 2011 na kuwa kiongozi wa chama chake bungeni.
Hazungumzii mambo binafsi
Mwezi Juni mwaka huu Brüderle alivunjika mkono na mguu baada ya kuanguka. Amemaliza kipindi kirefu cha kufanya mazoezi ya kupata nafuu. Brüderle ameeleza kuwa alikereka kwa sababu ilimchukua muda mrefu kupona wakati alikuwa katikati ya kampeni. Yeye ni mwanasiasa kwa moyo wote na hapendi kusema chochote juu ya maisha yake binafsi. Kinachofahamika ni kwamba ameoa, ni mprotestanti na anaishi Mainz.
Wa mrengo wa kushoto na kushoto zaidi
Mwenyekiti msaidizi wa chama cha mrengo wa shoto, Sahra Wagenknecht (44) na kiongozi wa chama hicho bungeni, Gregor Gysi (65) hawaelewani vizuri na hawapendi kufanya kazi pamoja. Hata hivyo wao ndio wanaokiongoza chama katika uchaguzi wa mwaka huu. Wanashirikiana na timu ya wanachama wengine sita ili wasigombane bali waendeshe kampeni.
"Die Linken" katika maisha binafsi
Sahra Wagenknecht anafahamika kama mtu anayefanya mambo yake mwenyewe lakini katika maisha yake ya binafsi yeye ni mpenzi wa Oskar Lafontaine, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho. "Ninahitaji uhuru wangu. Nataka kuwa na muda wa kusoma na kutafakari," anasema Wagenknecht. Ni mtu anayeweza kuchambua mada tofauti na kufanya utafiti. Ana shahada ya uzamili na zamani alipenda kuwa mtafiti.
Mzungumzaji mahiri
Alipokuwa mtoto, Gregor Gysi alitafsiri filamu za kuchekesha za kutoka muungano wa Sovieti. Marafiki zake walifurahi, walipoona jina lake limeandikwa mwisho wa filamu. Lakini sasa anapenda zaidi kuzungumzia michezo ya kuigiza, kusoma chambuzi na kusikiliza muziki wa "Classic". Hivi sasa hawezi kufanya kazi kama zamani kwani ana matatizo ya moyo.