Wagombea 82 waliofutiwa matokeo wazuiwa kuondoka Kongo
9 Januari 2024Hayo yamejiri baada ya Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, kufuta matokeo ya wagombea hao, wakiwemo mawaziri, magavana wa mikoa, maseneta pamoja na wabunge, kwa tuhuma za udanganyifu, ufisadi na umiliki haramu wa vifaa vya kupigia kura.
Katika barua kwa Kurugenzi Kuu ya Uhamiaji (DGM), Firmin Mvonde, ambaye ni mwendesha mashtaka mkuu, ametaka watuhumiwa hao wazuiliwe kutoka nje ya mipaka ya Kongo. Barua nyingine ilitumwa kwa mwenyekiti wa CENI akiomba apatiwe nyaraka zote zilizompelekea kufuta matokeo ya wagombea hao.
Upande mwengine, baada ya kusikiliza hapo jana kesi kuhusu uchaguzi mkuu uliomrudisha tena madarakani Raïs Félix Tshisekedi, Mahakama ya Katiba iliomba mgombea Théodore Ngoy kutoa ushuhuda wa kutosha.
Hatua ya mahakama katika kesi hiyo inasubiriwa mwishoni mwa wiki hii.