Wafungwa 300 waachiwa huru Burundi kupunguza msongamano
23 Januari 2017Hatua hiyo ni katika utekelezaji wa msamaha wa rais Pierre Nkurunziza. Miongoni mwa walioachiwa huru ni pamoja na wale waliopatikana na hatia ya kujihusisha na vugu vugu la kupinga muhula wa tatu kwa rais huyo. Kuachiwa wafungwa hao pia ni moja ya vigezo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya ili irudi kuisaidia kifedha Burundi.
Mongoni mwa walionufaika na msamaha huo wa Rais ni pamoja na wale waliotimiza thuluthi tatu ya kifungo jela, waliohukumiwa kifungo cha chini ya miaka 5, na wale wote waliodhihirisha mwenendo mzuri walipo kuwa korokoroni.
Kuachiwa kwa wafungwa kufungua misaada Burundi
Wengi ya waloachiwa ni vijana, baadhi ya wanasiasa walioshiriki katika vugu vugu la kupinga muhula mwingine kwa Rais Pierre Nkurunziza. Na wengine walotajwa kuwa katika tabaka la wanasiasa. Waziri wa sheria Aimee Laurentine Kanyana amesema hatua hiyo ya kuwaachiliwa wafungwa itawahusu wafungwa takriban 2500 kote nchini na kwamba itasaidia kupunguza msongamano katika magereza.
''Kuna idadi kubwa ya wfungwa katika magereza lakini wengi ni wale ambao bado hawajahukumiwa, ambao hatua hii kamwe haitowahusu. Tunawataka wanasheria kukumbuka ya kuwa pindi mtu yuko jela, basi maisha yake ni kama yamesisima. Hivyo tunawataka kuwajibika kwa kushuhulikia kesi zao haraka iwezekanavyo''. Alisema Kanyana.
Kuachiwa wafungwa ni moja ya vigezo vilivyowekwa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya ili urudi kuisaidia kifedha Burundi. Na hii ni mara ya kwanza rais kuamrisha wafungwa wakiwemo wa kisiasa kuachiwa huru. Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanakadiria kuwepo na wafungwa takriban elf 10 katika gereza zote za Burundi, ambapo wanakabiliwa na msongamano na mazingira duni.
Mwandishi: Amida Issa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman