Wafahamu wagombea wakuu watatu wa urais Taiwan
12 Januari 2024Beijing inadai kuwa kisiwa hicho kinachojitawala ni sehemu ya himaya yake na imekuwa ikitishia kutumia nguvu kukihodhi ikiwa itahitajika. Lakini ni wagombea gani wanaochuana katika nafasi hiyo ya urais wa Taiwan na wana misimamo gani kuihusu China?
Uchaguzi huo unafuatiliwa mno kimataifa hasa kutokana na uwezekano wa kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika Mlango Bahari wa Taiwan. Lakini huko Taiwan kwenyewe, wapiga kura wanashughulishwa zaidi na masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku kama vile uchumi unaosuasua, gharama kubwa ya makazi pamoja na kitisho cha Beijing kwa kisiwa hicho.
Miongoni mwa wagombea watatu wa Urais yupo:
Lai Ching-te, ambaye anafahamika pia kama William. Kwa sasa ni makamu wa rais wa Taiwan kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo-(DPP), ambacho kinapinga vikali madai ya China ya kwamba kisiwa hicho ni sehemu ya himaya yake.
Miaka iliyopita, mwanasiasa huyo wa miaka 64 alijinasibu kama "mwanaharakati wa kupambania uhuru wa Taiwan," jambo lililopelekea ukosoaji mkubwa kutoka kwa serikali mjini Beijing.
China inapinga madai yoyote ya uhuru wa kisiwa hicho ambayo hutolewa na wanasiasa wa Taiwan na imekuwa ikilaani vitendo vya Taipei kuwa na mahusiano rasmi na nchi nyingine.
Kwa mara kadhaa, Beijing imekataa mapendekezo ya kufanya mazungumzo na Lai Ching-te na hata Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen. Lai amesema kuwa yuko tayari kuzungumza na China lakini sio kutupa kapuni haki ya Taiwan kujitawala yenyewe.
Lai Ching-te ni daktari aliyesomea masuala ya afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani, na amekuwa mtumishi wa umma kwa miaka 25 na ameshikilia nafasi mbalimbali kama mbunge na meya wa jiji la kusini la Tainan.
Katika utawala wake na Tsai, Taiwan iliagiza zaidi silaha kutoka Marekani, ambayo inalazimika kukipatia kisiwa hicho silaha zinazohitajika ili kujilinda. Iwapo Lai atachaguliwa kama rais, ameahidi kuimarisha ulinzi na uchumi wa taifa hilo la kidemokrasia na kuendeleza mwelekeo wa sera uliowekwa na Tsai Ing-wen.
Soma pia:Wagombea Urais Taiwan wachuana katika mdahalo kabla ya uchaguzi
Hou Yu-ih ambaye ndiye mgombea kutoka chama kikuu cha upinzani cha Taiwan
Kuomintang, au KMT, ambacho serikali yake ilijiondoa katika uongozi wa kisiwa hicho mnamo mwaka 1949 baada ya kushindwa vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya Chama cha Kikomunisti cha China.
KMT imekuwa na msimamo wa kirafiki China kuliko chama kilicho madarakani cha DPP, ingawa imekuwa ikikanusha vikali kuwa upande wa Beijing. Lakini kwa kawaida, chama hicho kina uunga mkono wazo la muungano na China, ingawa katika miaka ya hivi karibuni kimebadilisha msimamo wake ili kuakisi azma ya idadi kubwa ya watu wa Tawain ambao wanapendelea hali isalie kama ilivyo.
Awali, Hou alikuwa mkuu wa jeshi la polisi katika kisiwa hicho kabla ya kuanza kujihusisha rasmi na siasa mnamo mwaka 2010. Mwanasiasia huyo mwenye umri wa miaka 66 kwa sasa ni Meya wa jiji la New Taipei, nafasi ambayo alijiuzulu ili kupata nafasi ya kugombea urais.
Hou anajinadi kama mwanachama asiye wa kawaida wa KMT na amesema ikiwa atachaguliwa kuwa rais hatouungana na China huku akisisitiza kuwa mustakabali wa Taiwan unatakiwa kuamuliwa na watu wake.
Hou Yu-ih ameahidi kuimarisha ulinzi na kuanzisha upya mazungumzo na Beijing kupitia mahusiano ya kitamaduni na mashirika ya kiraia na amesema anao uwezekano mkubwa wa kuishawishi China kuja kwenye meza ya mazungumzo kuliko mpinzani wake Lai ambaye amekuwa akimtumu kuielekeza Taiwan vitani.
Soma pia: Tsai: Amani ni suluhisho kati ya Taiwan na China
Na mgombea wa tatu katika uchaguzi wa urais katika visiwa vya Taiwani ni:
Ko Wen-Je, ambaye anawakilisha chama kidogo cha Watu wa Taiwan, ambacho alikianzisha mnamo mwaka 2019. Ni Daktari wa upasuaji aliyejibwaga kwenye siasa na anafahamika zaidi kwa kuwa na kauli zilizo wazi. Msimamo wake ni wa wastani linapokuja suala la mahusiano kati ya Taiwan na Beijing.
Ko ambaye anajinadi kuwa mwanasiasa ambaye atakubalika na Marekani na China, amesema pia kuwa tayari kufanya mazungumzo na Beijing lakini msingi wake utakuwa ni kudumisha uhuru na demokrasia vya Taiwan.
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 64 alikuwa meya wa Taipei kati ya mwaka 2014 na 2022 na hapo awali aliwahi kushirikiana na vyama vya DPP na KMT. Mpango wake na Hou wa kuwa na mgombea mmoja katika uchaguzi wa leo haukufanikiwa baada ya wawili hao kushindwa kuafikiana ni nani awe mgombea urais.
Ko ndiye mgombea maarufu zaidi miongoni mwa wapiga kura vijana wanaosifu ahadi zake zinazozingatia masuala muhimu kama vile elimu na gharama ya makazi.
Chanzo: APE