Wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais Senegal
24 Machi 2024Kampeni za uchaguzi zilipamba moto nchini Senegal zikijumuisha mikutano ya hadhara, misafara ya magari na hatua za nyumba kwa nyumba.
Mwaka huu, kutokana na kucheleweshwa kwa uchaguzi, ambao awali ulipangwa kufanyika Februari, wagombea urais walikuwa na muda mfupi wa kufanya kampeni kuliko ilivyo kawaida.
Wagombea 17 wa urais walikuwa na muda wa zaidi ya wiki mbili tu ili kuwashawishi wapiga kura zaidi ya milioni 7 wa taifa hilo la Afrika Magharibi waliojiandikisha.
Bassirou Diomaye Faye, mmoja wa wagombea wanaopigiwa upatu, amejikuta kuwa na muda mchache zaidi wa kufanya kampeni kwa kuwa alikuwa gerezani tangu Aprili mwaka 2023 na aliachiliwa tu kama sehemu ya mpango wa msamaha siku ya alhamisi iliyopita.
Faye mwenye umri wa miaka 49 alikuwa si maarufu sana nchini Senegal kabla ya kuungwa mkono na kiongozi mkuu wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye pia alifungwa gerezani mwaka jana na kuachiliwa Alhamisi ya Machi 14 pamoja na Faye.
Amadou Ba, ndiye mrithi anayependelewa na rais anaemaliza muda wake Macky Sall. Ba alijiuzulu wadhifa wake kama waziri mkuu ili kufanya kampeni za kuwania urais.
Idrissa Seck mwenye umri wa miaka 63 na waziri mkuu wa zamani aliyeshika nafasi ya pili mwaka 2019.
Khalifa Sall, 68, (ambaye si ndugu wa rais na ambaye aliwahi kuwa meya wa Dakar mara mbili).
Anta Babacar Ngom, mjasiriamali mwenye umri wa miaka 40, ambaye ndiye mwanamke pekee anayewania urais.
Fatou Sylla, ambaye anafanya kazi katika timu ya kampeni ya Ngom, ameiambia DW kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya Senegal bila kuwataja wanawake na vijana.
Uchaguzi wa kwanza katika mwezi wa ramadhan
Djibril Gninggue, mtaalam wa masuala ya Uchaguzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Watendaji wa Asasi za Kiraia nchini Senegal anaelezea changamoto zinazoukabili uchaguzi huu:
"Changamoto itakuwa kuendesha uchaguzi wa rais wa amani, wenye kuaminika na ulio wazi huku mchakato ukiheshimu kalenda ya uchaguzi."
Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika katika kipindi cha mwezi mtukufu wa ramadhan. Iman Moctar Ndiaye kutoka Msikiti Mkuu wa Liberte 6 katika mji mkuu wa Senegal Dakar aliwaonya watu kuendelea kuheshimu kanuni za mwezi mtukufu wa ramadhan wakati wa kampeni na kuwaambia wasiharibu funga yao kwa kutoa kauli za matusi au kufanya vitendo ambavyo vitahatarisha amani ya kijamii na utulivu wa nchi.
Soma pia: Sonko azungumza na wafuasi wake baada ya kuachiliwa huru
Wakati huo huo, mtaalam wa masuala ya uchaguzi El Hadji Saidou Nourou Dia anaamini kwamba itakuwa changamoto kubwa kufikia idadi kubwa ya watu watakaojitokeza kupiga kura katika mwezi huu wa Ramadhan.
Uamuzi wa dakika za mwisho wa rais anayemaliza muda wake Macky Sall mwezi Februari wa kuahirisha uchaguzi huo, ulizusha vurugu zilizosababisha vifo vya watu wanne katika nchi ambayo kwa kawaida huchukuliwa kama kinara wa utulivu na demokrasia katika eneo la Afrika Magharibi.
Senegal ni miongoni mwa nchi chache za Kiafrika ambazo hazikushuhudia mapinduzi tangu ilipojinyakulia uhuru wake mnamo Aprili 4, mwaka 1960. Nchi hiyo masikini ambayo asilimia 41 ya raia wake ni vijana, inakabiliwa na idadi kubwa ya vijana hao kujaribu kuihama nchi na kuelekea barani Ulaya.