Wachumi walia na Serikali ya Zuma
17 Aprili 2013Sekta ya viwanda vya kuunganisha magari nchini Afrika Kusini inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi hiyo ambapo kiasi cha dola za Marekani bilioni mbili kimewekezwa katika sekta hiyo. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wana wasiwasi kwamba serikali ya Afrika Kusini, ambayo imekuwa ikitoa ruzuku kubwa kwa sekta hiyo kupitia mifumo mbalimbali, imekuwa ikiisaidia sekta ambayo haisaidii kutengezea ajira.
"Ukiangalia kwa mtazamo mpana, utaona kuwa kuna viwanda vingine vingi hapa nchini ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza ajira kwa wananchi kulikoni Viwanda hivyo vya kuunganisha magari, kama viwanda cha nguo, kilimo, kusindika chakula na fanicha.'' Anasema Mike Schussler, Afisa Mtendaji mkuu wa Kampuni ya ushauri ya economists.co.za.
Ruzuku kwa sekta ya magari imekuwa ikitolewa kupitia programu ya muda mrefu ya maendeleo ya sekta ya magari, ambayo iliboreshwa mwaka huu wa 2013, na kuitwa Programu ya uendelezaji wa utengenezaji magari (APDP).
Schussler anaeleza kwamba wakati wafanyakazi wa sekta ya magari wanahitaji ujuzi na mafunzo vya hali ya juu, kuna sekta nyingine zinazohitaji wafanyakazi wasio na ujuzi mkubwa sana, akitolea mfano wa sekta ya utalii katika maeneo ya vijijini, ambayo haihitaji watu kuwa na ujuzi mkubwa sana.
Wakati mshauri wa masuala ya uwekezaji na biashara kutoka kampuni ya ushauri ya Cova nchini humo, Duane Newman, akisema kuwa ni muhimu sana kwa serikali ya Afrika Kusini kuwa na sekta ya viwanda vya kuunganisha magari inayoheshimika duniani, na kwamba serikali ilikuwa sahihi kuendelea kutoa msaada kwa sekta hiyo, aliongeza pia kuwa kunaweza kuwepo na mjadala kuwa sekta hiyo ilipewa msaada zaidi ya inavyostahili.
Alisema msaada kwa sekta hiyo ulifikia karibu dola bilioni mbili, karibu asilimia 20 ya msaada serikali ya Afrika Kusini inaoutoa kwa viwanda vyote vya ndani.
Johan Van Zyl, rais wa kampuni ya Toyota ya Afrika Kusini, ambaye pia ni afisa mtendaji mkuu wa Toyota Afrika na rais wa chama cha watengenezaji magari nchini Afrika Kusini, aliliambia shirika la habari la IPS kuwa msaada wa serikali umekuwa muhimu katika upanuzi wa sekta hiyo tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.
Zyl anasema ruzuku kwa sekta hiyo ilikuwa ni muhimu kwa sababu ni chanzo cha teknolojia mpya na uwekezaji, na muhimu zaidi, ajira zenye ujuzi. Anasema jambo hili linakwenda sambamba na malengo ya serikali ya kukuza uchumi kwa njia tofauti na zile zilizozoeleweka, ambako kuna uhamishaji mdogo wa maarifa na ongezeko la thamani. Zyl pia alipingana na hoja ya Schussler kwamba sekta hiyo inatengeneza ajira chache.
Naye Jeff Osborne, afisa mtendaji mkuu wa chama cha wauzaji wa magari nchini Afrika Kusini, ambacho kinawakilisha makampuni yanayouza magari, mafundi na matawi mengine yanayoshughulika na huduma kwa wateja katika sekta ya magari, kuongezeka kwa uwekezaji na watengenezaji wa magari nchini humo, kunaweza ishara ya imani katika nchi hiyo.
Alisema wakati utengenezaji wa magari unachangia kutoa ajira 25,000, sekta ya vipuri vya magari inajiri watu 60,000, na bishara ya rejareja ya magari inatoa ajira pia kwa watu wengine 30,000. Osborne anasema mtu anapaswa kuiangalia sekta nzima linapozungumziwa suala la ajira, na si sehemu moja tu ya utengenezaji.
Mwandishi: Hashim Gulana
Mhariri: Ssessanga Iddi Ismail