1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachimbaji migodi 33 waokolewa Chile

14 Oktoba 2010

Baada ya siku 69, hatimaye wachimbaji migodi 33 wa Chile, wameokolewa katika operesheni iliyotajwa kama ya miujiza.

https://p.dw.com/p/PdoV
Wachimbaji migodi waokolewa Chile.Picha: AP

Nchini Chile wachimbaji migodi wote 33 waliokuwa wamekwama kwenye mgodi wa San Jose wameokolewa. Watu kote duniani walifuatilia kwa makini shughuli hiyo ya uoakoaji wa wachimba migodi hao 33, waliokuwa wamenaswa chini ya ardhi kwa muda wa siku 69. Luis Urzula mwenye umri wa miaka 54, ndie alikuwa mtu wa mwisho kuokolewa kutoka kwenye mgodi huo, katika operesheni iliyojulikana kama 'Phoenix' iliyochukua saa 22, na kumalizika leo alfajiri.

Mgodi huo wa San Jose uliporomoka Agosti tarehe 5. Waokoaji walitumia sehemu ya roketi yenye ala iliyowanyanyua wachimba migodi hao, kwa kuwapitisha kwenye njia ya mwamba wa mawe. Viongozi kote duniani wameipongeza shughuli hiyo ya uoakoji nchini Chile, huku Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akiitaja kama miujiza mkubwa. Wachimbaji migodi hao ambao walikwama chini ya ardhi kwa muda wa zaidi ya miezi miwili, wanaendelea kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.