Wachezaji chipukizi wa kutizamwa kombe la dunia la Qatar
Kombe la Dunia mara nyingi hutoa fursa kwa vijana walio na talanta bora kuonyesha ujuzi wao. Ingawa wachezaji kama Jamal Musiala na Bukayo Saka wanajulikana sana, lakini michuano ya Qatar itawaibua vijana wapya.
Jamal Musiala, 19 (Ujerumani)
Musiala amekuwa sura mpya ya mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia Ujerumani. Licha ya umri wake, nyota huyo wa Bayern Munich anaonekana kuwa na nafasi kubwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu yake nchini Qatar. Akiwa na urefu wa futi 6 (mita 1.82), ni mpiga chenga mzuri, mfungaji na hodari wa kutoa pasi, ambaye ameonyesha kuwa hana hofu kwenye majukwaa makubwa zaidi.
Gavi,18 (Uhispania)
Ubora wa Gavi, mchezaji wa kimataifa wa Uhispania mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea, umemfanya ajiweke kama mtu muhimu kwa nchi yake. Mchezaji huyo wa Barcelona ni mpiga chenga na mtoa pasi mzuri wa mpira, kiasi cha kufananishwa na magwiji wa Uhispania Andres Iniesta na Xavi. Wakati mabingwa wa 2010 wakipanga njama za kurejea kileleni, Gavi ndiye kiongozi wa kizazi kipya.
Bukayo Saka, 21 (England)
Saka alipata uzoefu wake wa kwanza wa mashindano ya kimataifa kwenye Euro 2020, ambapo aliaminiwa kwa penalti muhimu dhidi ya Italia kwenye fainali. Tangu wakati huo amekua mwenye kujiamini zaidi na mwenye ushawishi mkubwa, licha ya kuteswa na mashambulizi ya kibaguzi yaliyofuata. Winga huyo wa Arsenal ni mmoja wa wachezaji chipukizi wenye vipaji katika kikosi cha Uingereza.
Takefusa Kubo, 21 (Japan)
Akitajwa "Messi wa Kijapani," mpiga chenga wa mguu wa kushoto wa Real Sociedad huwa anavutia kumtizama lakini sio mzuri kila wakati na anahitaji kufunga mabao mengi. Nchini Qatar, Japan inatumai kuwa ubunifu wa Kubo unaweza kuwasaidia katika kundi linalojumuisha miamba Uhispania, Ujerumani na Costa Rica.
Eduardo Camavinga, 20 (Ufaransa)
Camavinga alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Angola na wazazi wa Congo lakini alihamia Ufaransa akiwa na umri wa miaka 2. Kiungo huyo mahiri wa kati anayeweza kupiga chenga na kutoa pasi za uhakika, alikuwa sehemu ya timu ya Real Madrid iliyoshinda taji la ligi ya mabinbwa Ulaya UEFA Champions League mwaka wa 2022. Atakuwa mchezaji muhimu katika kutetea taji la Les Bleus nchini Qatar.
Rodrygo, 21 (Brazil)
Rodrygo ni mmoja kati ya wachezaji chipukizi wa Brazil wenye vipaji muhimu vya kushambulia. Ingawa anaweza kuona jukumu la kuanza kuwa gumu akiwa kando na washambuliaji mahiri, mshambuliaji huyo mchanga inaipa Selecao kitu cha ziada: jicho la ubunifu na nafasi za kufunga. Anapopata nafasi, mshambuliaji huyo wa Real Madrid anaweza kuwa vigumu kumwacha.
Gio Reyna, 20 (Marekani)
Erling Haaland, ambaye timu yake ya Norway haikufuzu michuano ya Kombe la Dunia, alimtaja mchezaji mwenzake wa zamani wa Borussia Dortmund Gio Reyna kama "ndoto ya Marekani." Reyna ni mchezaji wa kiwango ambaye analeta mabadiliko mengi kwenye safu ya ushambuliaji ya Marekani. Ukiacha majeraha, ambayo mara nyingi yamemuweka nje, atakuwa sehemu muhimu ya kampeni ya Marekani huko Qatar.
Felix Afena-Gyan, 19 (Ghana)
Afena-Gyan alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kiwango chake msimu uliopita, baada ya kupandishwa kutoka timu ya vijana hadi kwenye kikosi cha wakubwa cha AS Roma. Mshambuliaji huyo wa Ghana anasifika kwa kasi ambayo mara nyingi huwasumbua mabeki. Umbo lake dogo linamfanya linamfanya mwepesi kufika sehemu nyingi uwanjani na mtu anayefikiria kwa haraka.
Anis Ben Slimane, 21 (Tunisia)
Kiungo wa kati ambaye Tunisia watamtegemea kuisaidia safu yao ya ushambuliaji ni Slimane ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Denmark lakini akawa mchezaji wa Tunisia mwaka wa 2019. Mchezaji huyo wa Brondby ataleta ubunifu wake akilenga kupata bao Qatar wakati Watunisia wakiwinda kwa mara ya kwanza kufuzu hatua ya 16 bora katika kundi moja na Ufaransa, Australia na Denmark.