1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Wabunge waanzisha uchunguzi wa kumuondoa Biden madarakani

14 Desemba 2023

Wabunge nchini Marekani wamepiga kura kuanzisha rasmi uchunguzi wa kumuondoa madarakani Rais Joe Biden, na hivyo kuzidisha hali ya mvutano kati ya WaRepublican na Wademocrats kabla ya uchaguzi wa hapo mwakani.

https://p.dw.com/p/4a8rl
USA US-Kapitols in Washington, DC
Bendera ya Marekani ikipepea nje ya jengo la Baraza la Congress (Capitol) mjini Washington. Picha iliyochukuliwa 24.10.2023Picha: Pat Benic/UPI Photo/IMAGO

Huku wakizingatia shughuli zenye utata za Hunter Biden mtoto wa rais, wanachama wa Republican bado hawajatoa ushahidi unaohusu vitendo vya ufisadi vya rais Biden, na hivyo Baraza la Seneti linaloongozwa na Wademocrats halitaweza kumtia hatiani hata kama uchunguzi huo ungewezesha kuanzishwa kwa kesi halisi ya kumshtaki.

Kumekuwepo madai ya utovu wa nidhamu katika masuala ya fedha yanayotolewa na chama cha Republican ambao wanatumia fursa hii mpya kama jukwaa la kumshambulia Biden ambaye amekuwa katika kampeni za kuwania muhula wa pili madarakani. Lakini pia hatua kama hii inalenga kufifisha kesi za jinai zinazomkabili mpinzani wake wa karibu Donald Trump.

James Comer - Jamie Raskin / Untersuchung zur Amtsenthebung des Repräsentantenhauses
Mbunge wa Kentucky James Comer (kulia) akiwa na Mbunge Jamie Raskin wakati wa mjadala mnamo Septemba 28, 2023 kuhusu kuanzisha uchunguzi wa kumuondoa madarakani rais Biden.Picha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

Wabunge 221 WaRepublican wamepiga kura ya kuunga mkono hatua hiyo ambayo ilipingwa na wale wa Democrats wapatao 212. Wahafidhina wanamtuhumu mtoto wa kiume wa Biden Hunter kwa kutumia vibaya ushawishi wake hasa kwa kutumia jina la familia katika shughuli zake za kibiashara nchini Ukraine na China. Ikulu ya White House imekuwa mara kadhaa ikieleza kuwa madai hayo yanahusu matukio ya kabla ya Biden kuwa rais, na hivyo kusisitiza kuwa hakuna makosa yoyote yaliyofanyika kisheria.

Soma pia:Wabunge wa chama cha Republican huenda wakatafakari hatua ya kufanya uchunguzi juu ya  kumwondoa madarakani rais Joe Biden  

WaRepublican wameisifia hatua hiyo na kusema ni muhimu na kwamba kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakikusanya ushahidi wa kutosha. James Comer, ni Mbunge wa Republican kutoka Kentucky:

 "Nafikiri, tumewasilisha kwa uwazi kabisa hoja yetu leo. Ushahidi uliowekwa wazi umeonyesha mwelekeo wa kutatanisha mno wa familia ya Biden. Tumetumia miezi kadhaa ya uchunguzi na kukusanya ushahidi. Tuna swali rahisi ambalo nadhani Wamarekani wengi sana wajiuliza pia. Je, familia ya Biden walifanya nini hadi kupokea makumi ya mamilioni ya dola kutoka kwa maadui zetu kote duniani ?"

Kauli ya Biden baada ya kura hiyo ya Bunge

USA Präsident Joe Biden | Ukraine-Hilfen
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Yuri Gripas/ZUMA Wire/IMAGO

Biden amevunja ukimya wake mara baada ya kura hiyo ya Bunge na kuwashutumu WaRepublican kwa kuepuka masuala muhimu kama upatikanaji wa fedha kwa matumizi ya serikali na kusema wanachokizingatia ni kujipatia manufaa ya kisiasa kabla ya uchaguzi.

Biden amesema katika taarifa kuwa: " Badala ya wao kufanya kila waliwezalo ili kuboresha maisha ya Wamarekani, wao wanalenga kunishambulia kwa uwongo. Kuliko kushughulikia yanayohitaji kufanywa haraka, wamechagua kupoteza muda kwa harakati hizi za kisiasa zisizo na msingi ambazo hata WaRepublican wenyewe katika Baraza la Congress wanaafiki kuwa hazina ukweli wowote."

Chama cha Republican kilianza kuchunguza uwezekano wa kumuondoa madarakani Biden mapema mwaka huu na vikao vilianza mwishoni mwa mwezi Septemba, na hatimaye kufikia uamuzi wa kuandaa kura ya Bunge hapo jana. Katiba ya Marekani inatoa uwezo kwa Baraza la Congress kumuondoa rais madarakani kwa makosa yaliyothibitishwa ya uhaini, hongo au uhalifu mwingine mkubwa. Lakini hadi sasa hakuna rais wa Marekani aliyewahi kuondolewa madarakani kwa mchakato huo.

(Chanzo: AFP)