Wabunge wa Chadema walioapishwa wakaidi mwito wa chama
27 Novemba 2020Wabunge hao ambao wanashutumiwa kutokana na hatua yao ya kwenda bungeni ikiwa kinyume na msimamo wa chama hicho, hawakutokea kabisa mbele ya kamati ya chama hicho inayokutana Bahari Beach nje kidogo tu ya jiji la Dar es salaam.
Hakuna taarifa iliyofafanua kwa kina sababu za wabunge hao kugomea mwito wa chombo hicho kikuu ndani ya chama, ingawa kumekuwa na sababu za hapa na pale zinazoibuka kutoka ndani ya kikao hicho kilichoketi kuanzia saa tano asubuhi.
Waandishi wa habari waliopiga kambi kwenye eneo hilo wanasema kuwa hadi Ijumaa jioni hakuna kiongozi yeyote aliyetoka nje kutoa angalau muktasari wa yale yanayoendelea ndani ya kikao.
Kikao hicho kinaongozwa na mwenyekiti wake, Freman Mbowe na kuhudhuria na wajumbe wegine kadhaa akiwamo, Katibu wake, John Mnyika. Wabunge hao walishindwa kufika mbele ya kamati hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa baraza la wanawake wa chama hicho Bavicha, Halima Mdee ambaye amekuwa akikosolewa vikali na baadhi ya wanachama wa mabaraza ya wilaya yanayoweka shinikizo ang'olewe uanachama.
Haijulikani kama wabunge hao waliogoma kufika mbele ya kamati hiyo kama bado wameendelea kubaki Dodoma walikoapishwa wiki iliyopita au wamerejea katika maeneo yao.
Baadhi ya duru za habari zimekuwa nikinuu vyanzo mbalimbali vya habari vinavyoeleza sababu za wabunge hao kutofika kwenye kikao hicho.
Hili ni jaribio la kwanza kwa kamati kuu ya chama hicho kuona baadhi ya wanachama wake wanaopaswa kufika mbele yake kushindwa kutokea. Hadi Ijumaa jioni, kamati hiyo ilikuwa bado ikiendelea na mkutano wake wa ndani na kulingana na uzoefu wa vikao vya namna hii huenda kikao hiki kikaendelea hadi usiku.
Wachambuzi wa mambo wanasubiri kuona namna kamati hiyo itakavyofikia maamuzi yake ambayo pia yatatoa mwelekeo mwingine kuhusu chama chenyewe chenye mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa katika uchaguzi uliopita.
Kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani, Chadema imekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi uliopita wa Oktoba 28 ikisema sehemu kubwa ya matokeo hayo yalichakachuliwa.