Wabunge Uingereza wajipanga kumdhibiti Waziri Mkuu Johnson
4 Septemba 2019"Utulivu...waliosema ndiyo upande wa mkono kulia ni 328, waliosema hapana upande wa kushoto ni 301. Hivyo wa ndiyo wameshinda, wa ndiyo wameshinda. Imepita!" Usiku wa Jumanne (3 Septemba), Spika John Bercow wa Bunge la Uingereza alitangaza kile wachambuzi wanachokiita kipigo kibaya kwa Waziri Mkuu Johnson dhidi ya harakati zake za kuiondowa Uingereza iwe iwavyo kutoka Umoja wa Ulaya.
Kura hiyo ilimaanisha kwamba sasa waziri mkuu huyo mwenye mtazamo mkali dhidi ya Umoja wa Ulaya asingekuwa na nafasi ya kuendelea na mpango wake wa kuiondowa Uingereza kwenye Umoja huo bila ya kwanza kufikiwa makubaliano.
Ilimaanisha pia kwamba uchaguzi wa mapema si jambo lisilowezekana tena.
Baina ya Johnson na kiongozi mkuu wa upinzani, Jeremy Cobyn wa chama cha Labour, majibizano yalikuwa makali zaidi baada ya kura yenyewe, huku Johnson akimshutumu Corbyn kuwa dhaifu mbele ya matakwa ya Brussels na Corbyn akimtuhumu Johnson kwa kutaka kuiburuza Uingereza kibabe.
"Kila mtu anajuwa kwamba ikiwa mheshimiwa hapo atakuwa waziri mkuu, atakwenda Brussels kuomba muda zaidi. Atawakubalia na kukubali kila Brussels itakachodai," alidai Johnson.
Uchaguzi mpya?
Siku ya Jutamano (4 Septemba) wabunge walioshinda kura ya jana walitazamiwa kuwasilisha mswaada wa kuizuwia serikali ya Johnson kuitoa Umoja wa Ulaya bila makubaliano. Corbyn alisema hawaogopi kitisho cha waziri mkuu huyo kutangaza uchaguzi mpya endapo wabunge hao wangelishinda.
"Hakuna ridhaa kwenye bunge hili ya kuondoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano. Ikiwa anataka kupendekeza uchaguzi mkuu, sawa, lakini kwanza mswaada wa kuondoa uwezekano wa kutoka Umoja wa Ulaya bila makubaliano uletwe hapa," alisema Corbyn.
Kwenye masoko ya fedha, hivi leo sarafu ya Uingereza, paundi ya Sterling, ilipanda thamani yake kwa asilimia 0.5 ikiuzwa kwa dola 1.215 ya Kimarekani na asilimia 0.4 kwa euro, ambapo inauzwa kwa senti 90.78 kwa muda huu.
Uchaguzi mpya, hata hivyo, utazidi kupungua imani ya wawekezaji na kufungua uwezekano mpya wa kuporomoka kwa sarafu hiyo.