Wabunge Poland waidhinisha sheria ya kutolewa fedha za EU
13 Januari 2023Wabunge nchini Poland wameopiga kura kuidhinisha sheria mpya kuhusu uwajibikaji wa mahakama ambayo serikali inatumai itatimiza matarajio ya Umoja wa Ulaya na kusaidia kutolewa kwa mabilioni ya euro ya ufadhili wa kujikwamua kutokana na janga la UVIKO nchini humo.
Bunge limepiga kura 203 dhidi ya 52 huku wabunge 189 wakijiepusha na kuidhinisha sheria hiyo mpya, kura ambayo inaonyesha migawanyiko ndani ya muungano tawala na mashaka ya upinzani.
Serikali ya muungano wa siasa za mrengo wa kulia inasema vipengele vya sheria hiyo mpya vilikubaliwa na Brussels na kwa hiyo vinapaswa kusaidia kutolewa euro bilioni 35 za msaada wa Umoja wa Ulaya na mikopo. Baadhi ya mabadiliko ya awali yaliyofanywa na Poland hayakuuridhisha Umoja wa Ulaya. Umoja huo ulisitisha msaada kwa Poland, ukisema sera za serikali za kuweka udhibiti kwa idara ya mahakama ni ukiukaji wa misingi ya kidemokrasia.