Waasi watwaa ngome za serikali Syria
1 Agosti 2016Matangazo
Kituo cha kijeshi cha waasi kinachojumuisha kundi jipya lenye itikadi kali la Jabhat Fatah al Sham, kimetangaza kudhibiti maeneo ya kijeshi ya serikali Kusini Magharibi mwa mji wa Allepo, katika saa za kwanza za oparesheni ya kusitisha kuzingirwa kwa maeneo ya waasi na vikosi vya serikali.
Aidha serikali ya Syria imethibitisha mashambulizi hayo kupitia kituo cha habari cha kitaifa lakini ikasema vikosi vyake vimefanikiwa kuwasogeza waasi kando na kambi ya kijeshi, huku ikikanusha taarifa ya kutekwa shule ya Hikma na waasi hao.
Bado robo ya milioni ya raia wanaishi katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani Mashariki mwa mji wa Allepo, mji uliozingirwa kuanzia jeshi lililosaidiwa na vikosi vya kijeshi vya Iran lilipoziba barabara ya kuingia katika miji ya waasi mapema mwezi Julai.
Aleppo, moja ya miji mikubwa nchini Syria kabla ya kuanza machafuko miaka mitano iliyopita umegawika kati ya vikosi vya serikali na waasi tangu kipindi cha kiangazi mwaka wa 2012. Aidha Kuudhibiti tena mji huo itakuwa ushindi mkubwa kwa serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria tangu Urusi ilipojiunga na serikali ya Syria katika vita hivyo mwaka uliopita.
Siku ya Alhamisi, serikali ya Assad na mshirika wake Urusi walitangaza oparesheni ya pamoja katika eneo lililozingirwa kwa kutoa vijikaratasi vinavyowataka wapiganaji kusalimu amri na raia kuondoka katika maeneo hayo.
Hata hivyo serikali ya Marekani imetilia shaka hatua hiyo na kusema huenda ikawa ni mipango ya kupunguza idadi ya watu mjini Allepo, eneo muhimu kwa upinzani nchini humo ili iwe rahisi kwa serikali kuudhibiti tena.
Marekani yatangaza kuchukuwa sehemu kubwa ya Manbij
Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa vikosi vinavyoongozwa na Marekani ametangaza kuchukua udhibiti wa takriban asilimia 70 ya mji wa Manbij kaskazini mwa Syria kutoka kwa waasi wa Dola la Kiislamu (IS) baada ya kupiga hatua muhimu mnamo siku mbili zilizopita.
Jeshi la Waasi wa Syria wajulikanao kama Syrian Democratic Forces, likishirikiana na wanamgambo wa kikurdi YPG pamoja na wapiganaji wa kiarabu walianzisha kampeni miezi miwili iliyopita wakiongozwa na jeshi maalum la Marekani kupambana na wanamgambo wa IS katika eneo la mpakani mwa Syria na Uturuki.
Huku raia 2,300 wakiripotiwa kuutoroka mji wa Manbij, maelefu ya wakaazi bado wamekwama mjini humo. Hata hivyo, kuwepo kwa wakaazi katika mji huo waliokuwa wanazuwiwa kuondoka na wanamgambo wa IS kulitatiza kwa kiwango fulani mashambulizi ya angani ya Marekani hii ikiwa kwa mujibu wa duru kutoka kwa vikosi vya Kikurdi.
Aidha wanaharakati wanasema wakaazi kadhaa wameuwawa mjini humo kufuatia mashambulio ya angani katika eneo la Kaskazini huku shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International likisema muungano unaoongozwa na Marekani lazima ufanye kila juhudi kuzuwiya mauaji ya raia.
Mwandishi : Amina Abubakar/AFP/REUTERS
Mhariri: Daniel Gakuba
Matangazo