1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi washambulia Aleppo, Putin asita kushambulia upya

29 Oktoba 2016

Waasi Syria wamefanya mashambulizi makubwa yakilenga kuvunja mzingiro wa mwezi mmoja masahriki mwa Aleppo, wakati mshirika wa utawala wa Syria Urusi ukichelea kuendelea na mashambulizi mapya ya angani katika mji huo.

https://p.dw.com/p/2RrfP
Syrien Aleppo Offensive der Rebellen
Picha: Getty Images/AFP/O. Haj Kadour

Mapigano makali, mashambulizi ya makombora na miripuko ya mabomu ya kutegwa ndani ya magari viliutikisa mji huo wa kaskazini na kuuwa wanajeshi wa utawala wasiopungua 18 na wapiganaji washirika, kulingana na shirika la uagalizi wa haki za binaadamu, ambalo hata hivyo halikuweza kutoa idadi ya vifo kwa upande wa waasi.

Mji wa Aleppo ambao wakati mmoja ulikuwa mji mkubwa zaidi wa kiuchumi nchini Syria, umeharibiwa na mgogoro huo ulioanza mwezi Machi 2011 kwa maandamano ya kuipinga serikali na hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 300,000. Udhibiti wa mji huo, uliogawika kati ya upande unaodhibtiwa na waasi mashariki na magharibi ikiwa mikononi mwa vikosi vya Assad, ni muhimu katika kurejesha udhibiti wa Syria kaskazini.

Mashambulizi ya waasi siku ya Ijumaa yamekuja zaidi ya miezi mitatu tangu serikali ilipoanzisha juhudi za kuyazingira maeneo ya Aleppo mashariki ambako watu zaidi ya 250,000 wanaishi, na wiki kadhaa baada ya jeshi kuanzisha operesheni inayonuwia kuurejesha mikononi mwake upande unaoshikiliwa na waasi mashariki.

Makundi ya waasi "yanatangaza kuanza kwa mapambano ya kuvunja mzingiro wa Aleppo," alisema Abu Yusuf Muhajir, kamanda wa kijeshi na msemaji wa kundi la Ahrar al-Sham. Mshambulizi hayo "yatakomesha ukaliaji wa utawala katika upande wa Aleppo magharibi na kuvunja mzingiro kwa watu waliokwama ndani," aliliambia shirika la habari la AFP.

Mapigano yalikuwa yaliendelea hadi Ijumaa usiku magharibi na mashariki mwa Aleppo, lakini yalipungua makali, kulingana na mwandishi wa AFP katika maeneo ya waasi.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, wa Syria Walid al-Muallem na wa Iran Javad Zarif wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Ijumaa.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, wa Syria Walid al-Muallem na wa Iran Javad Zarif wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Moscow siku ya Ijumaa.Picha: Reuters/S. Karpukhin

Jeshi la Urusi lataka kurejelea mashambulizi

Moscow inasema haijaishambulia Aleppo tangu Oktoba 18 lakini jeshi la Urusi lilisema siku ya Ijumaa kuwa limemuomba rais Vladmir Putin kutoa idhibi ya mashambulizi ya angani kurejea tena. Lakini msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov alisema Putin "anaichukulia hatua hiyo kuwa isiyofaa kwa wakati huu," na kuongeza kuwa rais huyo alidhani ni muhimu "kuendeleza usitishaji mapigano wa kibinaadamu" katika mji huo ulioharibiwa vibaya na vita.

Licha ya msaada wa mashambulizi ya angani kutoka kwa Urusi, utawala wa Syria umepata mafanikio kidogo katika jitihada zake za kuiteka Aleppo nzima. Marekani iliutuhumu utawala huo siku ya Ijumaa kwa kutumia njaa kama zana ya kivita -- jambo ambalo ni uhalifu wa kivita chini ya mikataba ya Geneva -- na kuongeza ukosoaji dhidi ya Assad na waungaji wake mkono Urusi.

Akipinga madai ya Urusi kwamba mashambulizi dhidi ya Aleppo yamekoma, afisa wa serikali ya Marekani aliliambia shirika la AFP "utawala umakataa maombi ya Umoja wa Mataifa kufikisha msaada Aleppo mashariki -- ukitumia njaa kama silaha ya kivita".

Wiki iliyopita Urusi ilitekeleza mpango wa usitishaji mashambulizi ilioutaja kuwa wa "kibinadamu" wenye lengo la kuwaruhusu raia na waasi wanaojisalimisha kuondoka upande wa mashariki. Lakini ni wachache sana waliofanya hivyo, na mpango wa Umoja wa Mataifa kuondoa majeruhi ulishindwa kwa sababu usalama haukuweza kuhakikishwa.

Wakati waasi wakianzisha mashambulizi yao ya kwanza makubwa, shirika la uangalizi wa haki za bindaamu lilisema raia wasiopungua 15, akiwemo mwanamke na watoto wawili, waliuawa, na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika mashambulizi ya waasi Aleppo Magharibi.

Shirika hilo liliripoti makabiliano makali katika maeneo mbalimbali katika kingo za magharibi na kusini mwa Aleppo Magharibi, ambapo magari matatu ya waripuaji wa kujitoa muhanga yalilenga kituo cha ukaguzi katika eneo la Dahiyet al-Assad.

Ngome za serikali zalengwa pia

Waasi pia walizilenga ngome za serikali mashariki mwa Aleppo na katika mkoa wa pwani wa Latakia, kikiwemo kituo cha kijeshi cha Hmeimim kinachotumiwa na vikosi vya Urusi vinavyousaidia utawala. Mwandishi wa shirika la AFP Aleppo Mashariki alisema mashambulizi ya waasi yaliongeza morali huko, ambapo misikiti ilitangaza "Allah ndiye mkubwa zaidi" kupitia vipaza sauti.

Alisema wakaazi walichoma matairi ili kuunda moshi na kuweka kizuwizi dhidi ya mashambulizi ya angani. Mvua kubwa ziliuzima moto huo lakini pia zilikwamisha operesheni za angani za jeshi la Syria, na kuunda kile ambacho mmoja wa waasi alikitaja kuwa "ukanda mtakatifu usiyoruhusiwa kuruka ndege."

Mkuu wa sera ya kigeni na usalama wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini anakwenda Iran na Saudi Arabia kuzungumzia vita nchini Syria.
Mkuu wa sera ya kigeni na usalama wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini anakwenda Iran na Saudi Arabia kuzungumzia vita nchini Syria.Picha: DW/B. Riegert

Shirika la uangalizi lilisema waasi pia walifyatua maroketi dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi wa Nairab na uwanja wa kimataifa wa Aleppo, vyote vikiwa mashariki mwa mji na vinadhibitiwa na serikali. "Kuvunjwa kwa mzingiro hakuepukiki," alisema Yasser al-Yusuf, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya kundi la waasi la  Nuredine al-Zinki.

Kwa upande wake, televisheni ya serikali ilisema "jeshi limetibua njama ya magaidi kuushambulia mji wa Aleppo kutokea pande kadhaa kwa kutumia mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga". Shirika la habari la serikali SANA lilisema ndege za serikali zilikuwa zinafanya mashambulizi kusini na magharibi mwa Aleppo.

Umoja wa Ulaya ulisema Ijumaa kuwa mwanadiplomasia wake wa juu kabisaa Federica Mogherini alikuwa naelekea nchini Iran na Saudi Arabia kwa ajili ya mazuungumzo kuhusu vita hivyo vya miaka mitano.

Shinikizo hilo la kidiplomasia linakuja wakati kukiwa hakuna mataumaini ya kukomeshwa kwa mgogoro huo ulioziweka nchi hizo kubwa kabisaa kikanda katika pande pinzani, ambapo Iran inamuunga mkono Assad na Saudi Arabia ikiwa muungaji mkono muhimu kwa waasi wanaopambana kumng'oa madarakani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Isaac Gamba