Waasi wa Syria waingia mji wa Hama
6 Desemba 2024Wizara ya Ulinzi ya Syria ilisema hapo jana kwamba kumekuwapo na makabiliano makali kati ya jeshi na wale iliowaita magaidi, lakini magaidi hao walifanikiwa kujipenyeza kwenye mji huo muhimu.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, jeshi liliamriwa kuondoka na kujipanga sehemu nyengine ili kuepuka mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.
Soma zaidi: Nani anadhibiti eneo gani nchini Syria?
Kwa siku kadhaa sasa, waasi na wanajeshi wa serikali wamekuwa wakipambana kwenye mji huo wenye wakaazi milioni moja.
Hama ni mji wa pili mkubwa kutwaliwa na waasi kufuatia uvamizi wao wa ghafla ulioanza wiki iliyopita, ambapo pia wameutwaa mji muhimu wa kaskazini magharibi, Aleppo.
Mkuu wa shirika linalofuatilia vita vya Syria, Rami Abdel Rahman, amesema waasi hao wamewafungulia mamia ya wafungwa, wengine wakiwa wamekaa jela tangu mwaka 2011.